WHO yasema surua imeongezeka duniani | Masuala ya Jamii | DW | 14.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

SURUA

WHO yasema surua imeongezeka duniani

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limetangaza kwamba maambukizi ya ugonjwa wa surua yameongezeka mara tatu mnamo miezi saba ya mwanzo ya mwaka huu wa 2019, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Taarifa ya shirika hilo iliyotangazwa jana jioni (Agosti 13) mjini Geneva imesema mnamo miezi saba ya manzo ya mwaka huu wa 2019, visa vya maambukizi ya surua vilikuwa 364,808, ikiwa karibu mara tatu ya visa 129,239 vilivyokuwa vimetokea katika kipindi kama hicho mwaka uliopita wa 2018.

Msemaji wa WHO, Christian Lindmeier, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo mwaka huu ndicho cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka 2006.

Kinachotia wasiwasi zaidi, limesema shirika la afya ulimwenguni, ni kwamba kati ya visa 10 vya maambukizi ya surua ni kimoja tu kinachoripotiwa, ikimaanisha kuwa idadi halisi ya maambukizi ni kubwa zaidi kuliko iliyotangazwa rasmi.

Wasiwasi mwingine wa WHO unahusiana na kuongezeka kwa upinzani wa jamii dhidi ya chanjo.

Ugonjwa wa surua ambao unaambukizwa kwa kasi, unaweza kuepukwa kikamilifu ikiwa mtu atapewa dozi mbili za chanjo yake. Lakini mnamo miezi ya hivi karibuni, WHO imetoa tahadhari juu ya kudorora kwa shughuli za chanjo.

Mataifa ya Afrika yaongoza kwa surua

Symbolbild | Masern Impfung (imago/blickwinkel)

Chanjo ya surua, Masern.

Tangazo la jana la WHO limesema nchi zinazoongoza kwa maambukizi ya surua mwaka huu ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Ukraine. Nchi nyingine zilizoandikisha idadi kubwa ya wagonjwa wa surua ni Angola, Cameroon, Chad, Khazakhstan, Nigeria, Ufilipino, Sudan na Sudan Kusini.

Nchini Marekani hali pia sio shwari, kwana mwaka huu tayari imerikodi maambukizi 1,604 ya surua, wakati mwaka mzima wa 2018 ilikuwa na maambuzi 372 tu ya ugonjwa huo. Katika nchi za Umoja wa Ulaya, surua iliongezeka zaidi ya mara kumi, kutoka visa 84,462 mwaka 2018 hadi karibu 90,000 mnamo miezi saba ya kwanza ya mwaka huu.

Ugonjwa wa surua ambao unaweza kuuwa, ulikuwa umemalizika kabisa katika nchi zenye mifumo imara ya afya. Lakini, vuguvugu linalotumia madai potofu kwamba chanjo ya MMR dhidi ya ugonjwa huo inasababisha udumavu wa akili ya watoto, limepunguza sana utashi wa wazazi kuwapa chanjo watoto wao.

Katika tangazo lake la jana, WHO ilisisitiza kuwa chanjo dhidi ya surua iko salama kabisa, na inazuia kikamilifu maambukizi ya ugonjwa huo, na kuhimiza kila mtu kuhakikisha kwamba chanjo yao dhidi ya surua haijapitwa na wakati.
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com