1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle aihimiza Tunisia Kuepuka yanayotokea Misri

15 Agosti 2013

Westerwelle ameitumia ziara yake kutowa mwito wa kupatikana azimio la haraka kuutatua mgogoro wa kisiasa Tunisia ambako pia serikali inayoongozwa na wenye itikadi kali inapambana kubakia madarakani

https://p.dw.com/p/19QcJ
Waziri mkuu Ali Larayedh wa Tunisia na waziri wa nje wa Ujerumani Guido Westerwelle
Waziri mkuu Ali Larayedh wa Tunisia na waziri wa nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle anakutana na waziri mkuu wa Tunisia katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo (15.08.2013). Ziara ya Westerwelle imegubikwa na ghasia zinazoshuhudiwa nchini Misri lakini waziri huyo wa Ujerumani ameitumia nafasi hiyo kutowa mwito wa kupatikana azimio la haraka kuutatua mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia ambako pia serikali inayoongozwa na wenye itikadi kali inapambana kubakia madarakani.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesisitiza kwamba kinachotokea Misri kinapaswa kuzuiwa kutokea Tunisia nchi ambayo ni kitovu cha wimbi la kudai demokrasia lililopiga katika ulimwengu mzima wa Kiarabu.Tunisia ilikuwa nchi ya kwanza ya kiarabu kuuondowa utawala wa kiimla wa rais Zine El Abidine Ben Ali Januari mwaka 2011. Hapo jana baada ya kukutana na rais Moncef Marzouki Westerwelle alizungumzia msimamo wa nchi yake kuhusu hali ya kisiasa katika Tunisia na kusema kwamba

Westerwelle na rais Moncef Marzouki
Westerwelle na rais Moncef MarzoukiPicha: picture-alliance/dpa

''Tunisia sio Misri na kwa hivyo ni muhimu kwetu sisi kuona kwamba yanayotokea nchini Misri hayatoshuhudiwa katika Tunisia.Harakati zilizoonekana katika kipindi cha saa chache zilizopita za kuanza ukurasa mpya na kujumuisha vyama vyote vya kisiasa hilo ndilo suala muhimu na ndilo tunaloliunga mkono kwa njia za kidiplomasia tukiwa hapa Tunisia.Sisi kama Umoja wa Ulaya na kama Ujerumani tuna maslahi makubwa na hatuwezi kuona nchi jirani na sisi hazina usalama wa kutosha,na utulivu na pengine hata kitisho kipya cha ugaidi.Hilo ni suala linalotupa wasiwasi mkubwa na ndio sababu ni vyema pia tukajihusisha na hususan katika eneo hili.''

Nchi za Magharibi zimekuwa ziliiunga mkono Tunisia katika kipindi chake cha mpito kilichozingatia demokrasia lakini katika muda wa zaidi ya miazi sita nchi hiyo imetumbukia katika wimbi la machafuko na ghasia baada ya mauaji ya wanasiasa wawili wa upinzani,wote ikidaiwa wameuwawa na makundi ya itikadi ya kiislamu.Upinzani ulioanzisha maandamano tangu Julai 25 siku aliyouwawa Mohammed Brahmi kiongozi wa Upinzani,unaitaka serikali hiyo ya mpito ijiuzulu madarakani,hatua ambayo inapingwa na chama cha Ennahda kinachoihodhi serikali hiyo

Watunisia wamekuwa wakiandamana kudai serikali ijiuzulu
Watunisia wamekuwa wakiandamana kudai serikali ijiuzuluPicha: Reuters

.Leo mwenyekiti wa chama hicho ameyakataa mapendekezo ya upinzani ya kutaka paundwe baraza la mawaziri la watu wasiokuwa na vyama akisema kinachotokea nchini Misri kinatakiwa kuangaliwa kama funzo na Watunisia pamoja na kuwa chachu ya vyama nchini humo kushiriki katika mdahalo wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa taifa hilo.Mwenyekiti huyo wa chama cha Ennahda Rached Ghannouchi amesema anaweza kuridhia kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ikiwa vyama vyote vitaingia katika mazungumzo.Hata hivyo msimamo wake unatofautiana na naibu kiongozi wa chama hicho anayeunga mkono baraza la mawaziri wasiokuwa na vyama.Vyama vya Upinzani vinasema vitakaa chini na Ennahda pale tu serikali ya mpito itakapo vunjwa.

Mwandishi Saumu Mwasimba/dpa/Reuters

Mhariri:Josephat Charo