1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani ajiuzulu

8 Aprili 2019

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kujiuzulu kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kirstjen Nielsen, hatua inayosititiza nia yake ya kuimarisha sera ya uhamiaji

https://p.dw.com/p/3GRpu
USA, Washington: Kirstjen Nielsen, Heimatschutzministerin der USA
Picha: picture-alliance/dpa/E. Vucci

Kuondoka kwa Nielsen kunahitimisha mahusiano magumu na bosi wake, ambaye alisemekana kutokufarishwa na utendaji kazi wake licha ya utiifu mkubwa kwake na kuzitetea kikamilifu nyingi ya sera tata za rais huyo.

Wakati wa uongozi wake wa miezi 18 katika wizara hiyo nyenye nguvu, Nielsen mwenye umri wa miaka 46 alitambulika sana kwa utaratibu wenye utata wa kuwatenganisha watoto na wazazi wao, na hivyo kulengwa mara kwa mara na makundi ya haki na chama cha upinzani cha Democratic ambacho kila mara kilitoa wito wa kumtaka ajiuzulu.

Hayo yote, inaonekana hayakumridhisha Trump ambaye aliandika jana kwenye Twitter kuwa waziri wa usalama wa ndani Kirstjen Nielsen ataachia wadhifa huo, na akamshukuru kwa kazi yake.

USA, Washington: Kevin McAleenan
McAleenan ndiye kaimu waziri wa usalama wa ndaniPicha: picture-alliance/AP/A. Brandon

Aliongeza kuwa Kamishna wa Forodha na Ulinzi wa Mipaka wa Marekani Kevin McAleenan atakuwa kaimu waziri kuchukua nafasi ya Nielsen. McAleenan ni afisa wa muda mrefu wa ulinzi wa mipaka ambaye anaheshimiwa sana na wabunge na ndani ya serikali.

Kwenye barua yake ya kujiuzulu, Nielsen alisema kuwa licha ya hatua zilizopigwa katika kuufanyia mageuzi usalama wa ndani, umefikia wakati wa yeye kujiuzulu.

Hatua hiyo imekuja siku mbili tu baada ya yeye na Trump kuzuru kwa pamoja eneo la mpaka wa Mexico jimbo la California, ambapo rais altoa ujumbe mkali kwa wanaopanga kuwa wahamiaji haramu na waomba hifadhi akisema kuwa Marekani imejaa.

Licha ya onyo la kutokea madhara makubwa ya kiuchumi, hata kutoka kwa viongozi wakuu wa chama chake cha Republican, Trump mara kwa mara ametishia kuufunga mpaka wa Marekani na Mexico, akilitaka Bunge la Marekani na serikali za nchi za Amerika ya Kati kuchukua hatua za kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji ambao ulimfanya Nielsen wiki iliyopita kuamuru kuongezwa haraka idadi ya wahudumu ili kuishughulikia hali hiyo.

Makadirio ya Doria za Mpakani yanaonyesha kuwa idadi ya wahamiaji wanaopita kwenye mpaka wa Mexico ilkuwa Zaidi ya 100,000 mwezi Machi, wengi wao kutoka El Savador, Honduras na Guatemala. Kwa mujibu wa Nielsen, hiyo ni idadi kubwa kabisa kuwahi kusajiliwa kwa mwezi katika karibu muongo mmoja. Trump alipunguza msaada katika nchi hizo tatu mwezi uliopita kutokana na mminiko huo wa wahamiaji.