1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani Malaysia akutwa na hatia

Daniel Gakuba
28 Julai 2020

Waziri mkuu wa zamani wa Malaysia, Najib Razak, amekutwa na hatia katika mashtaka yote saba ya ufisadi unaOhusiana na kashfa ya mabilioni ya dola yaliyokuwa yametolewa na serikali kwa ajili ya mradi wa maendeleo.

https://p.dw.com/p/3g1Wo
Malaysia Najib Razak vor Gericht in Kuala Lumpur
Picha: Reuters/Lim Huey Teng

Jaji wa Mahakama Kuu ya Kuala Lumpur; Mohamad Nazlan Mohamad Ghazali, amepitia hoja zote zilizowasilishwa na timu ya utetezi ya Razak, na kumkuta na hatia ya mashtaka saba yaliyokuwa yakimkabili.

"Baada ya kuzingatia ushahidi wote katika kesi hii, naona kuwa upande wa waendesha mashtaka umethibitisha kesi yake bila ya shaka yoyote," amesema Ghazali.

Fedha hizo ziliibiwa na kuelekezwa katika matumizi binafsi, yakiwemo ununuzi wa magari ya anasa na kazi za sanaa zenye gharama kubwa.  

Akitoa hukumu hiyo Jumanne (Julai 28), Jaji Ghazali alisema upande wa waendesha mashtaka umeweza kutetea hoja yake vyema na kuondoa mashaka yote juu ya hatia ya Razak.

Kipimo cha utawala wa Malaysia

Hukumu hii dhidi ya Razak ilichukuliwa kama kipimo kwa utawala wa sheria nchini Malaysia, kwani imetolewa miezi mitano tu baada ya muungano unaokijumuisha chama chake kushinda uchaguzi. Wengi walihofu kuwa ushindi huo ungeshawishi uamuzi wa mahakama.

Soma zaidi: Malaysia: Waziri mkuu wa zamani ahojiwa kuhusiana na rushwa

Razak mwenye umri wa miaka 67, amekana madai yote katika kesi hiyo.

"Kwa kumalizia, baada ya kuzingatia ushahidi wote katika kesi hii, nimeona upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo," Jaji  Ghazali aliiambia Mahakama Kuu ya Kuala Lumpur.

Najib alionekana kuinamisha kichwa chini baada ya kusomewa mashtaka.

Nje ya mahakama hiyo, kulikuwa na mkusanyiko wa mamia ya wafuasi wake waliokuwa na hasira.