Waziri Kerry aipa matumaini Somalia | Matukio ya Afrika | DW | 05.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waziri Kerry aipa matumaini Somalia

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema Somalia inaelekea mustakabali bora, katika ziara ya kihistoria nchini humo tangu uingiliaji wa maagamizi kwa wanajeshi wa Marekani miongo miwili iliyopita.

Mwanadiplomasia huyo wa juu wa Marekani alitumia saa chache tu katika mji mkuu Mogadishu, na hakutoka nje ya uwanja wa ndege wa kimataifa wenye ulinzi mkubwa, ambako alikutana na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, na waziri mkuu Omar Abdirashid Ali Sharmake.

"Zaidi ya miaka 20 iliyopita, Marekani ililaazimika kuondoka nchini mwenu," alisema Kerry akimaanisha vita vya maafa vya 'Black Hawk Down' vya mwaka 1993, wakati wanajeshi 18 wa Marekani na mamia ya Wasomali walipouawa katika uingiliaji wa kijeshi na kiutu uliokwenda kombo. Waziri Kerry alisema ameitembelea Somalia leo kwa sababu nchi hiyo inabadilika na kuanza kushirikiana na jumuiya ya kimataifa.

Waziri Kerry akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mogadishu.

Waziri Kerry akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mogadishu.

Aahidi msaada zaidi kwa Somalia

Ziara ya Kerry imelenga kutoa msukumo wa kidiplomasia kwa serikali dhaifu ya Somalia, katika mapambano yake dhidi ya kundi la waasi wa Al-Shabaab, ambao licha ya kupoteza maeneo wameendelea kufanya mashambulizi nchini kote pamoja na mataifa jirani.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani alisema wakati akizungumza na rais Hassan Sheikh Mohamud, kwamba mara nyingine atakapokuja watakuwa na uwezo wa kutembea mjini Mogadishu, ambapo Sheikh Mohamud naye alimjibu kwamba mji wa Mogadishu umebadilika kwa sasa kuliko iliyokuwa miaka miwili iliyopita.

Kerry aliahidi msaada zaidi kwa Somalia, nchi ambayo imeharibiwa vibaya na vita na kuendelea kwa migogoro ya kibinaadamu, tangu kuanguka kwa utawala wa Siad Barre mwaka 1991. Kerry alizishukuru Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Uganda ambazo zimechangia wanajeshi kwa kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM, chenye jumla ya wanajeshi 22,000, ambao wanailinda serikali mjini Mogadishu na wanapambana dhidi ya Al-Shabaab.

Makao makuu ya AMISOM mjini Mogandishu.

Makao makuu ya AMISOM mjini Mogandishu.

Dola nusu bilioni kwa AMISOM

Maafisa wa Marekani wamesema tangu mwaka 2007, Marekani imetumia zaidi dola nusu bilioni katika ufadhili wa kikosi cha AMISOM, na kwa mujibu wa ofisi ya waandishi wa habari za uchunguzi, yenye makao yake mjini London na ambayo inafuatilia operesheni za siri za Marekani, nchi hiyo imefanya mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani dhidi ya wapiganaji wa Al-Shabaab katika kipindi sawa. mwezi Septemba, makombora ya Marekani yalimuuwa kiongozi wa Al-Shabaab Ahmed Abdi Godane.

Kerry pia alikutana na viongozi w amashirika ya kiraia ndani ya uwanja wa ndege, ambao ni jengo kubwa lililoko ufukweni mwa bahari wenye ulinzi mkali sana, na ambao ndiyo makao makuu ya vikosi vya AMISOM. Maafisa wengine wa ngazi ya juu wameitembelea Somalia katika miaka ya hivi karibuni, wakiwemo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Lakini ziara hizo zinakuwa za haraka na zinafanyika kwa usiri mkubwa kwa kuhofia mashambulizi ya Al-Shabaab.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.
Mhariri: Joseph Nyiro Charo