Wazimbabwe washerehekea kujiuzulu kwa Mugabe | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wazimbabwe washerehekea kujiuzulu kwa Mugabe

Shangwe na nderemo vilitawala katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare na kwingineko nchini humo mara tu baada ya Spika wa Bunge Jacob Mudenda kuisoma barua ya Rais Robert Mugabe kujiuzulu wadhifa wa rais ''kwa hiari yake''.

Simbabwe Rücktritt Robert Mugabe | Feier im Parlament (Getty Images/AFP/J. Njikizana)

Wabunge wakisherehekea baada ya Spika wao kusoma barua ya kujiuzulu kwa Rais Robert Mugabe

Tangazo hilo la kushtukiza lilisomwa katika kikao maalumu cha bunge na seneti, ambacho kilikuwa kimeanza mchakato wa kisheria ambao hatimaye ungemtimua Mugabe madarakani, baada ya kukaidi miito ya kujiuzulu kutoka chama chake mwenyewe, ZANU-PF. Usiku kucha watu wamesherehekea mitaani, huku magari yakipiga honi mfululizo.

Kwa kujiuzulu huko, utawala wa miaka 37 wa Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93 hatimaye umefika kikomo. Mugabe alisema katika barua yake ya kujiuzulu kwamba amefanya hivyo kwa kuzingatia maslahi ya taifa, na kupisha ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani.

Mwisho wa enzi

Simbabwe Mugabe bei TV-Ansprache (picture-alliance/AP Photo)

Robert Mugabe ameitawala Zimbabwe tangu mwaka 1980

Kama ishara ya kumalizika kwa enzi katika historia ya Zimbabwe, mtu mmoja aliiondoa picha ya Robert Mugabe katika chumba walimokuwa wakikutana wabunge, na mtu mwingine akaiweka mahali pake, picha ya aliyekuwa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa. Rais Mugabe alimfukuza kazi Mnangagwa wiki mbili zilizopita, hatua iliyochukuliwa kama kumtengenezea njia mkewe Grace kuwa mrithi wa kiti cha urais.

Hatua hiyo ilikuwa kosa ambalo baadaye limemuangusha kiongozi mkongwe. Chama cha ZANU-PF kimetangaza kwamba Mnangagwa asiyejulikana mahali aliko hivi sasa, atarejea nchini katika muda usiozidi saa 24, na kuapishwa kuwa rais wa mpito atakayeongoza kwa siku 90. Hayo aliyasema msemaji wa chama hicho Simon Khaya Moyo.

Kulingana na katiba ya Zimbabwe, makamu wa rais mpya Phelekezela Mphoko ndiye angepaswa kuapishwa kuwa rais kufuatia kujiuzulu kwa rais Robert Mugabe lakini duru za habari zinasema hayuko nchini humo.

Ujumbe watoka sehemu mbalimbali

Emmerson Mnangagwa Politiker aus Simbabwe (Getty Images/AFP/A. Joe)

Huyu ndiye Emmerson Mnangagwa anayetarajiwa kuwa rais wa mpito wa Zimbabwe

Pande mbali mbali zimekuwa zikitoa kauli kuhusu kujiuzulu kwa Rais Robert Mugabe. Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais wa Guinea Alpha Conde amesema amefurahi vilivyo kusikia kwamba Mugabe amekubali kujiuzulu, na kuongeza hata hivyo kuwa anasikitika kwamba Mugabe aliyemtaja kuwa shujaa wa Afrika, ameondoka kupitia mlango wa nyuma, akiwa ametupwa mkono na bunge lake.

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amewatahadharisha wananchi, kwamba demokrasia nchini Zimbabwe haiwezi kujengwa kupitia mchakato usio wa kidemokrasia.

Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza ambayo ni mkoloni wa zamani wa Zimbabwe, amesema kujiuzulu kwa Robert Mugabe kunatoa fursa kwa Zimbabwe kuchukua njia mpya ya uhuru na isiyo na ukandamizaji, nayo wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kujiuzulu huko ni tukio la kihistoria na nafasi kwa watu wa Zimbabwe kuitoa nchi yao katika kutengwa.

Jeshi la Zimbabwe ambalo kuchukuwa kwake udhibiti wa nchi wiki iliyopita kulianzisha mchakato wa kumuondoa Mugabe Madarakani, limehimiza utulivu na kuheshimu sheria wakati wa shamra shamra zinazoendelea. Kamanda wake mkuu, Constantino Chiwenga, amesema vitendo vyovyote vya fujo na ulipaji kisasi vitakabiliana na mkono mkali wa vyombo vya usalama.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, ape, dpae

Mhariri: Josephat Charo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com