1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Watu zaidi wakamatwa kuhusiana na shambulizi la Moscow

Tatu Karema
2 Aprili 2024

Idara ya usalama ya Urusi, FSB, inawashikilia watu zaidi ambao inawashuku kuhusika na shambulizi la kigaidi kwenye ukumbi wa tamasha wa Crocus Kaskazini-Magharibi mwa Moscow zaidi ya wiki moja iliyopita

https://p.dw.com/p/4eK5h
Mshukiwa wa shambulizi la kigaidi la mjini Moscow nchini Urusi afikishwa mahakamani mnamo Machi 23,2024
Mshukiwa wa shambulizi la kigaidi la mjini Moscow afikishwa mahakamaniPicha: Alexander Zemlianichenko/AP/dpa/picture alliance

FSB imesema Jumatatu kwamba raia wanne wa kigeni ambao walihusika moja kwa moja katika ufadhili na kuwapa vifaa magaidi, wamezuiliwa mjini Dagestan katika eneo la Urusi la Caucasus ya Kaskazini.

Soma pia:Urusi imekamata wapangaji wanne zaidi wa shambulio la Moscow

Vyombo vya habari vya serikali pia vilionesha video iliyotolewa na FSB ambapo mwanamume ambaye hakutambulishwa anasema aliwapa silaha wahalifu hao kwenye mji mkuu wa Dagestani, Makhachkala kufanya mashambulizi hayo katika ukumbi wa Crocus.

Hata hivyo, video hiyo haikuweza kuthibitishwa.

Washukiwa wengi pia wamekamatwa nchini Tajikistan.

IS yadai kuhusika na shambulizi la Moscow

Kundi la wanamgambo linalojiita dola la kiislamu IS limedai kuhusika katika shambulizi hilo la Machi 22 ambapo idadi ya waliofariki imetajwa kuwa takriban watu 144 huku zaidi ya 550 wengine wakijeruhiwa na baadhi wakiwa bado hawajulikani walipo.