1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu watatu wauawa Nyakach Kenya kufuatia shambulio la bomu

Musa Naviye8 Desemba 2021

Watu 3 akiwemo mshambuliaji wa kujitoa muhanga wameuawa kwenye tukio la mripuko wa bomu uliotokea katika kijiji cha Kamloma Kata ndogo ya Awach, huko Kisumu nchini Kenya usiku wa kuamkia Jumatano. 

https://p.dw.com/p/43z9Z
Kenia Tote bei Anschlag auf ein Dorf
Picha: Reuters/Stringer

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi kituo cha Katito, majira ya saa tatu na dakika 20 usiku wa  jumanne, naibu chifu kata ndogo ya Awach - James Okoth alipiga ripoti kuhusu tukio la shambulizi la kigaidi lililo waua watu wawili akiwemo mshukiwa wa kigaidi huku msichana wa miaka 14 akijeruhiwa kwenye tukio hilo.

Taarifa za polisi zimefafanua kuwa, mshukiwa anayekisiwa kuwa wa kigaidi John Odhiambo maarufu Pope alifika nyumbani kwa Petro Onyango na mkewe Mary Atieno akawapata na mtoto wao wa kike Nancy Aoko  na kuanza kuwauliza maswali kabla ya kilipuzi alichokuwa amebeba kulipuka, Mama mwenye boma na mshukiwa huyo walikufa papo hapo huku baba mwenye boma akifariki alipofikishwa katika hospitali ya eneo la Nyakach. Mtoto wao alipelekwa hospitali ya Katito akiwa katika hali mahututi.

Okoth ameeleza kuwa, mshukiwa huyo anarekodi ya hulka za kigaidi ikizingatiwa kuwa, mnamo tarehe 17 Disemba mwaka jana alilipua kilipuzi katika kituo cha kibiashara cha Katito akilenga kumua mpenzi wake ila alifanikiwa kukwepa mtego huo salama huku mshukiwa akikimbilia mafichoni kabla ya kuibuka tena na kufanya shambulio la sasa.

Kufuatia tukio hili, kamanda wa polisi jimbo la Kisimu Kipkirui Ngeno amesema, vikosi vya usalama vimeimarisha doria wakiendelea na uchunguzi zaidi kubaini sababu ya shambulizi la Nyakach.

Shambulizi hili limeibua hofu kubwa miongoni mwa wakaazi eneo hilo ambao wengi wao hawapo tayari kuzungumzia swala hilo.