1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kiasi 32 wauwawa Libya

Saumu Mwasimba
8 Aprili 2019

Maelfu ya watu wayakimbia maeneo ya karibu na Tripoli kufuatia mapigano makali kati ya jeshi la serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa na wanamgambo wanaoongozwa na jenerali Haftar

https://p.dw.com/p/3GS2g
Libyen Nationale Libysche Armee (LNA)
Picha: Reuters/E.O. Al-Fetori

Nchini Libya mapigano bado yanaendelea kati ya vikosi vya wanamgambo vya jenerali Khalifa Haftar na jeshi la serikali inayotambuliwa kimataifa. Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametowa mwito leo wa kusitishwa vita na kuwataka viongozi wa Libya kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Mpaka kufikia wakati huu kiasi watu 2,200 wameyakimbia mapigano kusini mwa mji mkuu wa Libya Tripoli tangu tarehe 4 kufuatia kuchacha kwa mapigano. Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo jumatatu inasema raia wengi wamenasa kwenye mapigano na wako katika hali ya kushindwa kupata huduma za dharura. Ni kufuatia hali hiyo ya kupamba moto mapigano Jumuiya ya Kimataifa inapaaza sauti kuzitaka pande zinazopigana kusitisha mapigano hayo. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametowa mwito mapigano yasitishwe kufungua njia kwa ajili ya huduma za kibinadamu. Mkuu huyo wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya pia amesema  mawaziri wa mambo ya nje wanaoukutana  Luxenmbourg katika mkutano wao wa kawaida wanatarajiwa kuunga mkono ujumbe huo.

Libyen Mitglieder der National Army LNA in Bengasi
Picha: Reuters/E. O. Al-Fetori

Jana Marekani nayo ilitowa mwito wa kumtaka jenerali Haftar na vikosi vyake kusitisha mara moja  mapigano.Mapigano yanaendelea ingawa leo imetajwa kwamba mashambulizi mazito yamepungua kiasi. Wanamgambo wa Haftar wamepania kuusogelea mji wa Tripoli licha ya Umoja wa Mataifa kutowa mwito wake wa kutaka mapambano yasitishwe. Jumapili vikosi vya Khaftari  na jeshi la serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa walikabiliana kwa mashambulizi ya angani ikiwa ni siku tatu baada ya Haftar kuanzisha operesheni ya kutaka kuudhibiti mji mkuu Tripoli ambao ni makao makuu ya serikali inayotambuliwa kimataifa.Msemaji wa jeshi la serikali inayotambuliwa yenye makao yake Tripoli Kanali Mohamed Gnounou amesema:

Libyen Mohamed Ghnouno GNA-Sprecher
Mohammed Ghnounou-Msemaji wa jeshi la LibyaPicha: Reuters/H. Amara

''Tripoli na miji jirani ilishambuliwa na vikosi vya Khalifa Haftar katika jaribio lililoshindwa la kutaka kuiondowa serikali halali.Vikosi vyake viliingia kutoka Shuwairf huko Mashariki na Kusini na kuingia Mezadh na Gharian. Mji wa Gharian ulishambuliwa jumatano ambayo ni Aprili 3. Tunasubiri kwa utulivu mkutano wa kitaifa wa Libya ambao ulikuwa ni matarajio ya walibya utakaoirudisha katika Usalama.''

Watu wasiopungua 32 wameuwawa na wengine kiasi 50 wamejeruhiwa kufuatia mapigano ya Liya katika maeneo ya karibu na mji mkuu Tripoli.Vikosi vya Haftar vimesema mpaka sasa wapiganaji wake 14 wameuwawa. Libya iko katika mgawanyiko tangu lilipoanza vuguvugu la kumuondowa madarakani Moammer Ghaddafi lililoungwa mkono na jumuiya ya NATO  mwaka 2011 lililosababisha hatimae kuodolewa madarakani na kuuwawa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu nchini Libya.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo