1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 40 wafa maji wakikimbia machafuko Msumbiji

5 Novemba 2020

Watu wapatao 40 waliokuwa wanakimbia mauaji yanayofanywa na makundi ya itikadi kaskazini ya Msumbuji wamekufa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama baharini katika kisiwa cha Ibo jioni ya siku ya Jumatano. 

https://p.dw.com/p/3ktAv
Mosambik Pemba | Geflüchtete Menschen | Paquitequete Strand (Delfim Anacleto/DW)
Picha: DW

Shirika la Habari la Ureno, Lusa, limeripoti kuwa boti iliyowachukua zaidi ya abiria 74 ilizama na kusababisha vifo vya watu 40, huku wengine 32 wakiokolewa.

Duru kutoka eneo la tukio zinasema boti hiyo iliyoanza kutoka mji wa pwani ya Msumbiji wa Palma ulio karibu na mpaka na Tanzania, ilipakia abiria hao 74 kwenye kitongoji cha Namandigo, na ilizama muda mfupi baadaye kufuatia kuzidiwa na wingi wa watu.

Kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo kwa kawaida boti hiyo hubeba watu 30.

Vifo vya watu 40 vimetokea wakati maelfu ya watu wanakimbia vurugu na mauaji yanayoendeshwa na wanamgambo wa itikadi kalikatika eneo la kaskazini la jimbo la Capo Delgado , huku wengi hutumia boti kyafikia maeneo salama.

Watu wengi wanakimbia machafuko kaskazini mwa Msumbiji

Mosambik Pemba | Geflüchtete Menschen | Paquitequete Strand (Delfim Anacleto/DW)
Wakaazi wa kaskazini mwa Msumbiji hutumia mashua na majahazi kukimbia machafuko Picha: DW

Takwimu za serikali kwenye mji mkuu wa jimbo hilo wa Pemba zinaonesha kuwa zaidi ya wakimbizi 12,000 wamewasili kwa boti 250 katika wiki mbili za mwisho za mwezi Oktoba huku nusu kati ya hao ni watoto.

Shirika la Madaktari wasio na mipaka limesema hadi sasa zaidi ya watu 400,000 wameyahama maakazi yao kaskazini ya Msumbiji kukimbia ukatili na mauaji ya makundi ya Itikadi kali

Mmoja wa raia wa Msumbuji aliyekimbia nyumba yake amesema "kwa sababu ya vita , niliondoka Macomia nikiwa na mimba ya miezi saba. Nilijificha msituni kwa siku nne bila chakula wala maji, niliondoka msituni baada ya waasi kuondoka eneo la Macomia "

Wanamgambo wauwa watu wengine kwa kuwachinja 

Kisa cha watu kufa maji kimetokea wakati washambuliaji wanaodhaniwa kuwa wanamgambo wa itikadi kali wamewauwa wanaume na wavulana kadhaa waliokuwa wakishiriki sherehe za jando kaskazini ya Msumbiji.

Mosambik Cabo Delgado | Angriffe von Islamisten
Wanamgambo wa itikadi kali huchoma moto vijiji Picha: AFP/M. Longari

Viongozi wa eneo hilo wamesema jana kuwa miili iliyokatwakatwa ya wanaume watano na wavulana 15 ilipatikana siku ya Jumatatu ikiwa imesambaa kwenye msitu mmoja uliopo wilaya ya Muidumbe.

Afisa mmoja kutoka wilaya jirani ya Mueda ambaye hakutaka jina lake kutajwa, amesema polisi iligundua kuhusu mauaji hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo waligundua kuwepo kwa miili ya watu.

Wanamgambo wa itikadi kali wanaondeshea operesheni zao kwenye eneo hilo la Msumbujiwalivishambulia vijiji kadhaa mwishoni mwa wiki iliyopita na kisha kupora mali pamoja na kuchoma maakazi ya watu kabla ya kukimbilia msituni.

Mamlaka za Msumbiji hazijatoa maelezo yoyote kuhusiana na kisa hicho kinachohushishwa na wanamgambo wa itikadi kali ambao kwa miaka mitatu sasa wanaitikisa nchi hiyo na hivi karibuni wamechukua udhibiti wa maeneo makubwa, huku wakiendelea kuua raia na wanajeshi wa serikali.