1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 16 wauwawa na waasi, Congo

21 Oktoba 2021

Watu 16 wameuwawa baada ya waasi kutoka Uganda ADF kukishambulia kijiji cha Kalembo katika wilaya ya Beni nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo usiku wakuamkia leo Alhamisi.

https://p.dw.com/p/41xeb
DRK Symbolbild FARDC
Picha: Alain Wandimoyi/AFP

Kisa hicho kimetokea katika wakati wabunge nchini Congo wamepitisha uamuzi wa kurefusha muda wa utawala wa kijeshi kwenye mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri. Soma Waasi wa ADF wauwa tena mashariki mwa DRC

Ni milango ya saa moja na nusu za usiku wa kuamkia leo alkhamisi,ndio waasi wa ADF walikishambilia kijiji cha Kalembo, kilomita arubaini mashariki ya mji wa Beni, kwenyi barabara inayoelekea Uganda. 

Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya simu, kiongozi wa tarafa ya Bulongo Arnold Isse Muyambo, akithibitisha ripoti hiyo mapema leo alisema  "Lilikuwa shambulizi la ADF,wanajeshi wetu wamefanya kazi hadi asubuhi ya leo na hadi sasa hatujapata taarifa kamili kuhusu matokeo ya awali. Hivi karibuni tutapata taarifa kamili ilikutoa mwangaza kuhusu kilichotokea ."

Nayo ripoti toka mashirika ya kiraia katika eneo la Kalembo zadokeza, kuwa watu kumi na sita waliuawa,maduka kuporwa pamoja na nyumba kadhaa kuchomwa moto na ADF. soma Waasi wa ADF wauwa watu 10 Beni nchini Kongo

Idadi ya waliouawa huenda ikaongezeka kwani harakati za kutafuta miili ya ziada bado zinaendelea.

Jeshi laomba ushirikiano

Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Na akizungumza na wanahabari kuhusu hali ya usalama katika eneo hili, msemaji wa jeshi katika operesheni dhidi ya ADF pamoja na makundi mengine ya waasi Sokola1, captain Anthony Mualushayi aliwaomba raia kuliunga mkono jeshi, ili kumtokomeza adui anayewauwa watu hapa kwa muda mrefu sasa. 

"Tunaomba raia watuunge mkono na wasife moyo. Adui anayo mikakati yake lakini kwa pamoja sisi jeshi na raia, tutafanikiwa siku moja kumtomeza adui ambae ameshasababisha vifo vingi na kwa muda mrefu." alisema captain Anthony Mualushayi.

Naye Anincet Bamuswekere wa shirika la kutetea haki za binaadamu PAIDC, kufuatia mauwaji pamoja na wakaazi kuyahama mashamba yao ya Cacao, anatoa mwito kwa serikali kupitia jeshi, kuwatokomeza ADF, ambao pamoja na kuwauwa watu, watapelekea watu kufa kwa njaa. Soma Tshisekedi aahidi kupambana na waasi wa ADF

Msururu wa mashambulizi

Symbolbild | DR Kongo | Anschlag der Alliierte Demokratische Kräfte Kongo
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mauwaji ya Kalembo katika wilaya ya Beni, ni moja wapo ya mlolongo wa mashambulizi yanayofanywa na ADF dhidi ya vijiji mbalimbali katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri. Soma Mauaji ya waasi wa ADF nchini DRC kupata suluhu?

Tangu mwanzo wa wiki hii, ni watu sichini ya hamsini waliouawa na ADF, wakati wabunge mjini Kinshasa, wanaendelea kuongeza muda kwa utawala wa kijeshi katika mikoa husika,bila ya kupendekeza hatua nyingine zinazodhaniwa kuwa huenda zikasaidia kuwatokomeza waasi wa ADF. 

Wakizungumza na DW pale wakitaka majina yao kutotajwa,baadhi ya wakaazi wa Beni waliiomba serikali ya Congo kuomba msaada wa kijeshi kwa nchi jirani kwani, jeshi la Congo lknaonekana kulemewa na hasa,wanajeshi wengi kwenyi operesheni, wameshapigana kwa muda mrefu bila ya kubadilishwa. 

 

John Kanyunyu, DW Beni