Waasi wa ADF wauwa watu 10 Beni nchini Kongo | Matukio ya Afrika | DW | 01.07.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waasi wa ADF wauwa watu 10 Beni nchini Kongo

Waasi wa ADF, wamewauwa watu 10 katika mjini Beni usiku wa kuamkia Alhamis na kuwateka watu tisa wakiwemo watoto. Mauwaji hayo yanatokea wakati mji wa Beni unakabiliana na mashambulizi ya mabomu ya kienyeji.

Sikiliza sauti 02:31

Waasi wa ADF wauwa watu 10 mjini Beni

Mauwaji hayo ambayo ni ya kwanza tena kutokea katika mji huu wa Beni baada ya zaidi ya mwaka mmoja bila ya ADF kuwauwa watu hapa mjini, yanakatisha tamaa,kwani yanafuatia pia mlolongo wa mashambulizi ya mabomu ya kienyeji.

ADF wanawauwa watu Beni, wakati eneo hili likiwa katika utawala maalumu, baada ya rais kutangaza hali ya hatari katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri.

Waasi wapokonywa silaha

Na akizungumza na wanahabari jana mjini Goma, gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Luteni Jenerali Ndima Kongba Constant alisema,kuwa tangu kutangazwa kwa hali ya hatari katika eneo hili, kuna kazi kubwa ambayo imefanywa na jeshi katika eneo la Beni.

Hapa gavana Ndima Constant anatupatia matokeo ya awali ya operesheni za kijeshi dhidi ya ADF.

"Magaidi arubaini na tisa waliuawa na tuliona miili yao, ADF kumi wakishikwa na wako mikononi mwa mahakama ya kijeshi. Kuhusu vifaa, tumechukua toka mikono ya waasi silaha ishirini na nne pamoja na risasi za silaha mbalimbali. Kuhusu operesheni, tumeteka na kudhibiti makambi muhimu ya ADF," alisema gavana Constant.

Waasi wafanya uharibifu ikiwemo kuchoma nyumba

Demokratische Republik Kongo Beni

Wanajeshi wa Kongo wakipiga doria mitaani

Tujulishe kwamba, tangu kutangazwa kwa hali ya hatari katika mikoa miwili ya nchi hii karibia myezi miwili sasa,waasi wa ADF nao wamezidisha mashambulizi yao dhidi ya maeneo mbalimbali, katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri.

Hapo Jumatano,waasi hao waliyachoma manyumba katika kijiji cha Idohu, katika wilaya ya Irumu, na majuzi tu, waasi hao waliwauwa watu sichini ya ishirini katika vijiji vingine vya wilaya ya Irumu, mkoani Ituri, na watu wengi wamepotea, na isijulikane waliko.

Matumaini ya wakaazi wa maeneo yanayoshuhudia vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na ADF, yakuona mauwaji pamoja na mashambulizi vinakomeshwa kupitia utawala maalumu wa kijeshi, yametoweka.

Hali katika mji wa Beni ni ya wasiwasi wakati huu, na mashule mengi yamewarejesha wanafunzi nyumbani.