Watu 11 wauawa kwenye mapigano mapya Kenya | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Watu 11 wauawa kwenye mapigano mapya Kenya

Watu watatu wametiwa mbaroni kuhusiana na ghasia zilizozuka upya katika kaunti ya Baringo eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya huku wananchi wakiiomba serikali kuimarisha usalama baada ya watu 11 kuuawa.

Miongoni mwa waliouawa katika mapigano mapya yaliyozuka wiki hii kati ya jamii ya Pokot na Ilchamus ni pamoja na watoto watatu na wanawake saba. Mapigano hayo yamezuka wiki mbili baada ya Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo kusimamisha shughuli zake kwa kuhofia usalama wa maafisa wake. 

Mapigano mapya yamezuka katika Kaunti ya Baringo licha ya kikosi cha maafisa wa usalama wapatao 2,000 kupelekwa katika eneo hilo wiki mbili zilizopita. Wakazi wa eneo hilo wameitaka serikali kuimarisha usalama.

Mapigano hayo yamezuka huku Rais Rais Uhuru Kenyatta akitoa Onyo kwa wanasiasa wanaochochea ghasia katika eneo la Bonde la Ufa. Rais Kenyatta alisema, ninanukuu ''tutatumia mbinu zote tulizonazo kuwaweka katika mkono wa sheria wote wanaohusika kuchochea mapigano hayo na nachukua fursa hii kuwaonya wanasiasa katika maeneo yaliyoathiriwa kukoma kuchochea mapigano ya aina yoyote kwani mtakabiliwa kisheria''.

Kenia Präsident Uhuru Kenyatta (Reuters/T. Mukoya)

Rais Uhuru Kenyatta

Tayari watatu wametiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo yaliyotokea usiku wa kuamkia jana. Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya ambalo wiki mbili zilizopita lilisimamisha shughuli zake za kusambaza misaada ya kiutu limeomba serikali kuu kutoa ulinzi kwa maafisa wake ili wasije wakashambuliwa tena wiki moja baada ya kurejea katika shughuli hizo.

Serikali imeorodhesha eneo la Baringo kuwa eneo hatari na kupeleka kikosi cha zaidi ya maafisa 2,000 wa usalama kuzima aina yoyote ya ghasia. Licha ya kikosi hicho cha usalama kupelekwa eneo hilo jamii zinazozozana bado zimeendeleza uhasama na kufanya mashambulizi tena.

Eneo la Baringo limekuwa likikumbwa na ghasia hasa kila wakati uchaguzi unapokaribia. Wanasiasa wa eneo hilo wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia.

 

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com