1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu waionya Congo kuwajumuisha waasi jeshini

24 Novemba 2022

Wataalamu wa masuala ya ulinzi wameitahadharisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya kuirejesha sera ya kuwajumuisha wapiganaji wa zamani ndani ya jeshi la taifa.

https://p.dw.com/p/4K1Mj
DR Kongo | kongolesische Soldaten auf dem Weg zur Front im Kampf gegen die M23-Rebellen
Picha: Arlette Bashizi/AFP/Getty Images

Tahadhari yao imetolewa wakati juhudi zinaendelea za kujaribu kumaliza mzozo unaochochewa na uasi wa kundi la M23. Kundi hilo lenye idadi kubwa ya wapiganaji wa kikongo wenye asili ya kabila la Tutsi limeanzisha tena hujuma yake hivi karibuni baada ya kuwa kimya kwa miaka kadhaa.

Wapiganaji wake waliingia msituni mwishoni mwa mwaka 2021, wakidai Jamhuri wa Demokrasi ya Congo imeshindwa kutimiza ahadi yake ya kuwajumuisha ndani ya jeshi la taifa, moja ya matwaka chungunzima ya kundi hilo.

Tangu wakati huo wapiganaji wa M23 wamekamata maeneo kadhaa makubwa mashariki mwa Congo, na sasa wanaukaribia mji wa kimkakati wa Goma.

Mnamo Jumatano wiki hii, serikali ya Congo na Rwanda -- taifa inalolituhumu kuwaunga mkono waasi waM23 -- zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano yatakayoanza kutekelezwa siku ya Ijumaa.

Hayo ni kulingana na Angola, nchi iliyobeba dhima ya kuwa mpatanishi wa mzozo uliopo kati ya Kinshasa na Kigali.

Wataalamu: Kuwajumuisha waasi jeshini siyo suluhu 

Hata hivyo katikati ya kutafutwa amani ya kudumu, wataalamu wa masuala ya ulinzi wameionya Congo dhidi ya kuwajumuisha waasi ndani ya jeshi wakisema hilo siyo suluhisho.

Demokratische Republik Kongo | Mai-Mai-Milizen
Picha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Jacques Djoli , mtaalamu wa masuala ya ulinzi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mbinu hiyo haijawahi kufanikiwa kuleta uthabiti na badala yake hulidhoofisha jeshi.

Ikifahamika na wengi nchini Congo kwa msamiati wa kifaransa "brassage" -- ikimaanisha mchanganyiko -- wazo la kuwajumuisha waasi ndani ya jeshi iliasisiwa mwaka 2003 mwishoni mwa vita vya pili vya Congo vilivyodumu kwa miaka mitano.

Viongozi wa Congo walisitisha sera hiyo mwaka 2013, wakisema haikuwa na mafaniki, lakini Djoli amekwenda mbali zaidi akisema utekelezaji segemnege wa sera hiyo ulipelekea jeshi kuvamiwa na askari wasio watiifu.

Katika baadhi ya wakati, waasi walioingizwa jeshini walionzisha uasi ndani ya chombo hicho. Mfano wa dhahiri ni katikati mwa miaka ya 2000, wapiganaji wa kundi la waasi la CNDP walianda kupambana na wanajeshi wenzao.

Waasi wanaweza kuongeza madai ya kujumuishwa serikalini

DR Kongo, Protest in Goma
Picha: Aubin Mukoni/AFP

Afisa mwengine wa masuala ya ulinzi aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina anakubali kwamba kuwaingiza waasi ndani ya jeshi kumepunguza uwezo wa chombo hicho. Mkosoaji mwingine wa sra hiyo ni Juvenal Munubo, mjumbe wa kamati ya ulinzi ya Bunge la Congo.

Amesema kuwachanganya waasi na wanajeshi kumesadifu kutoliimarisha jeshi la taifa au kulifanya kuwa tiifu kwa nchi akimaanisha kuilinda nchi na kuitii katiba.

Ana wasiwasi kwamba katika hali ya mzozo wa sasa, waasi wa 23 wanaweza kutumia fursa hiyo kudai kupatiwa nafasi pia ndani ya serikali.

"Itakuwa ni kosa la kihistoria kuwajumuisha M23 au makundi mengine ndani ya jeshi" amesema Munubo, akisema suluhisho pekee ni waasi kujisalimisha, kuwapokonywa silaha na kurejea kwenye maisha ya kiraia.