1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga vita mihadarati Afrika wakubaliana kuongeza nguvu

21 Septemba 2018

Wadau kutoka taasisi za kupambana na matumizi ya dawa za kulevya barani Afrika wamekubaliana kuongeza nguvu kisheria katika mapambano yao.

https://p.dw.com/p/35J2f
Tansania Repräsentanten im Kampf gegen Drogenmißbrauch
Picha: DW/H. Amri

Viongozi wa taasisi za kupambana na dawa za kulevya kutoka mataifa mbali mbali ya bara la Afrika Wamekubaliana kuongeza nguvu za kisheria na uwajibikaji katika kupambana na uchapushaji wa matumizi ya dawa za binadamu zinazosaidia kupunguza maumivu na kusababisha usingizi. Dawa hizo zinakuwa kama ni aina nyengine ya dawa za kulevya. Maafikiano hayo yanatokana na mkutano wao wa siku tano uliomalizika hii leo mjini Dar es Salaam. 

Mkutano ukiwa umeingia siku ya tano leo Ijumaa, hoja mbalimbali na changamoto katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu unaoambatana na biashara hiyo ikiwemo usafirishaji wa binadamu na utakasaji wa fedha vimejadiliwa kwa kina na viongozi hao na kuiona suluhu katika matumizi ya sheria zenye nguvu ya kufifisha kasi ya vigogo wa biashara hiyo yenye nguvu na mtandao mpana ulimwenguni.

Matumizi ya sheria na utashi kisiasa

Kamishna wa tume ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kutoka nchini Tanzania Siang'a, amewaambia waandishi habari kuwa, mbali na wajumbe wa mikutano kukubali matumizi ya sheria, utashi wa viongozi wa kisiasa, usiri uliopo pamoja na elimu isiyo na kukoma katika jamii ni sehemu ya makabiliano ya uhakika dhidi ya dawa za kulevya barani humo.

Wito umetolewa kwa wadau kufahamu kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya ni la kila taifa kwa maslahi ya watu wake
Wito umetolewa kwa wadau kufahamu kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya ni la kila taifa kwa maslahi ya watu wakePicha: bdnews24.com

Tamko la kisisasa la mwaka elfu mbili na tisa mbele ya Umoja wa Mataifa lililozitaka nchi wanachama kupambana vilivyo na biashara haramu ya dawa za kulevya, mkutano huu ikiwa ni sehemu ya kujitathmini kwa bara la Afrika katika kukabiliana na vita dhidi ya dawa hizo haramu na aina zote za uhalifu zinazoambatana na biashara hiyo ambapo kwa wastani wanakubali kuwa wapo katika nafasi nzuri ya mapambano.

Kugeuza dawa za matibabu kuwa kama mihadarati

Hili linatajwa kuongeza mbinu nyingine ya watumiaji wa dawa hizo, kubuni matumizi ya dawa za binadamu za kupunguza maumivu na zile za kuleta usingizi kuwa ni sehemu ya mbadala wa dawa hizo haramu za kulevya kutokana na urahisi wa upatikanaji wake katika maduka ya dawa jambo ambalo kila nchi imejizatiti katika kuchukua hatua madhubuti .

Tom Kalter ambaye ni kiongozi wa timu ya kupambana na dawa za kulevya na uhalifu kutoka Umoja wa Ulaya katika mkutano huo, amewataka viongozi hao kukumbuka kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya ni la kila taifa kwa maslahi ya watu wake, hivyo ni muhimu kuwa na ushirikiano usio na shaka, hiyo italeta matokeo yenye kupongezwa kwa ushindi dhidi ya vita hivyo vigumu.

Nchi zaidi ya hamsini zimeshiriki mkutano huo wa 28 zikiwemo Kenya, Malawi, Zambia,Nigeria,Uganda,Burundi na mwenyeji Tanzania.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman