Wanne washtakiwa kwa njama za kumuua rais Kagame | Matukio ya Afrika | DW | 22.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wanne washtakiwa kwa njama za kumuua rais Kagame

Washukiwa wanne wa uhaini nchini Rwanda walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kula njama za kufanya mauaji dhidi ya viongozi wa serikali ya Rwanda akiwemo rais Paul Kagame pamoja na kufanya mashambulizi ya kighaidi.

Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Mshukiwa mkuu katika kundi hilo, mwimbaji maarufu wa nyimbo za maridhiano nchini Rwanda Kizito Mihigo alikiri mashtaka yote yanazomkabili. Chumba cha mahakama kilijaa kupindukia na watu walilazimika kusimama nje na kuchungulia madirishani wakati kesi ikianza.

Maafisa wengi wa polisi walionekana kuwa na kazi ya ziada ya kuwapanga watu ambao mpaka walisogelea kabisa washukiwa waliosimama kizimbani.

Rais Kagame akisalimiana na wafuasi wake mjini Kigali.

Rais Kagame akisalimiana na wafuasi wake mjini Kigali.

Tuhuma dhidi ya washukiwa
Wote wanne walishtakiwa kwa kuhatarisha usalama wa serikali iliyoko madarakani au kufanya mauaji dhidi ya rais wa jamhuri, shitaka jingine ni ushirikiano kwenye kupanga na kujaribu kutekeleza vitendo vya ughaidi, lakini kwa upandewa Kizito Mihigo anashukiwa pia kuwa na mpango wa kufanya mauaji.

Baadaye kidogo washukiwa walipewa nafasi ya kukiri au kukataa mashitakaa hayo yanayowakabili. Mshukiwa mkuu kwenye kundi hili la watu wanne muimbaji mashuhuri Kizito alisema kuwa anakiri mashitaka yote aliyosomewa.

Lakini akaomba kwamba apewe muda wa wiki moja atafute wakili mwingine kwa sababu yule alokuwa naye mapema kabla ya kuingia mahakamani aliamueleza kwamba ameachana na kazi hiyo ya kumtetea.

"Kama nilivyosema awali ningependa nipewe muda wa kutafuta wakili maana yule niliyekuwa nimempata muda mfupi kabla ya kuja hapa alisema kwamba hayuko tayari kuendelea kunitetea."

Wakiri baadhi ya mashtaka
Washukiwa wenza mwanadada Agnes Niyibizi afisa mapokezi katika kampuni moja mjini Kigali, Cassian Ntamuhanga mkurugenzi mkuu wa zamani wa Radio moja binafsi mjini Kigali na Jean Paul Dukuzumuremyi, askari wa zamani katika jeshi la Rwanda wote walitangaza kukiri baadhi ya mashtaka yanayowakabili huku wakiyakana mengine ambayo hata hivyo hawakuyafafanua.

Wanyarwanda wamefanya maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Wanyarwanda wamefanya maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Wawili kati ya washukiwa wanne walitangaza kwamba watajitetea wao wenyewe huku wengine wawili wakiomba wapewe muda watafute mawakili. Kufuatia maombi hayo mkuu wa jopo la majaji Gasana Jean Damascene aliamuru kesi hiyo iahirishwe kutokana na ombi la washukiwa.

Washukiwa wote wanne walikamatwa wiki iliyopita kwa kile polisi ilitangaza kwamba kwa ushirikiano na makundi ya RNC na FDLR yanayoendesha harakati zake nje ya Rwanda walipanga kufanya mashambulizi makubwa mjini Kigali hususan kwenye jengo refu kuliko yote jijini Kigali maarufu kama KCT.

Mwandishi: Sylvanus Karemera
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman