Wanamgambo washambulia kituo cha usalama Pakistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wanamgambo washambulia kituo cha usalama Pakistan

Wapiganaji wa Taliban wamekishambulia kituo cha usalama nje ya uwanja wa ndege wa Karachi nchini Pakistan, ikiwa ni siku moja baada ya shambulizi la usiku kucha lilofanywa na wanamgambo hao kuwaua watu 37

Tukio hilo la leo limekuja ndege za kijeshi za Pakistan kufanya mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Taliban karibu na mpaka wa Afghanistan. Shambulizi hilo la wataliban karibuni katika uwanja wa ndege lilizusha maswali zaidi kuhusiana na uwezo wa serikali kuvidhibiti vituo vyake kutokana na kitisho cha Taliban, na limetokea wakati ndege za kivita zikidondora mabomu katika maeneo yanayoshukiwa kuwa maficho ya wanamgambo hao kaskazini magharibi mwa Pakistan, na kuwaua watu 25.

Shambulizi la leo katika kituo cha usalama lililenga eneo la kuingia katika kambi ya Jeshi la Usalama wa Uwanja wa ndege – ASF karibu kilometa 500 kutoka uwanja wenyewe wa ndege, na karibu kilomita moja kutoka eneo wanakopitia abiria. Polisi na wanajeshi walikimbilia eneo hilo lakini maafisa wameripoti kuwa hakujakuwa na waathirika wowote na kuwa hawakufyatuliana risasi na wapiganaji hao.

Angriff auf den Flughafen von Karachi 10.06.2014

Taliban ilidai kuhusika na shambulizi la uwanja mkuu wa ndege wa Karachi, Pakistan

Safari za ndege zimerejea tena baada ya kusitishwa kwa muda kwa mara ya pili. Pakistan iliingia katika mazungumzo na Taliban mnamo mwezi Februari mwaka huu na pande hizo mbili zikakubali kusitisha mapigano mwezi Machi, ambayo kisha yalivunjika mwezi mmoja baadaye.

Mchambuzi wa masuala ya usalama Hasan Askari anasema kipindi cha mazungumzo hayo kiliwapa nafasi Wataliban kujiimarisha tena, wakati serikali ikiendelea kuyumbayumba kuhusiana na hatua ya kuchukua. Waangalizi wengi wanaamini kuwa mchakato wa amani umekufa na kwamba serikali ni lazima sasa ichukue hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuishambulia ngome ya Taliban ya Waziristan Kaskazini. Kumekuwa na uvumi wa kufanyika operesheni katika eneo hilo lakini wachambuzi wanasema haijawa wazi kama jeshi lina uwezo wa kufanya mashambulizi hayo bila ya msaada wa kutoka upande wa mpaja wa Afghanistan ambako wanamgambo wanaweza kutorokea kama watashambuliwa.

Wakaazi wa eneo hilo wamekuwa wakihama kutokana na vijikaratasi vilivyosambazwa wiki iliyopita na mbabe wa kivita Hafiz Gul Bahadur, ambaye anaonekana kuwa ni mwendani wa Pakistan wakati akiyafanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa NATO katika nchi jirani Afghanistan. Bahadur aliwataka wakaazi kuondoka majumbani mwao kwa sababu serikali inaweza kuanza opersheni ya mashambulizi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com