1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ethiopia walizingira eneo la Tigray

17 Februari 2026

Wasiwasi wa kuzuka upya vita kati ya jeshi la Ethiopia na vikosi vya Tigray umetanda, kila upande ukijikusanya kwenye maeneo ya mpakani

https://p.dw.com/p/58vUK
Jeshi la TPLF likionesha nguvu zake kwenye gwaride mjini Mekelle
Jeshi la TPLF likionesha nguvu zake kwenye gwaride mjini MekellePicha: Million Haileslassie/DW

Wanajeshi wa Ethiopia na vikosi vya Tigray wamekusanyika kwenye eneo la mpaka la Kaskazini mwa jimbo la Tigray, hatua ambayo imeongeza khofu ya kuzuka upya kwa vita katika eneo hilo.

Chanzo kimoja cha kidiplomasia kutoka nchi za Magharibi kilichozungumza na shirika la habari la AFP leo Jumanne, kimesema wanajeshi wa serikali ya Ethiopia wanalizingira jimbo la Tigray wakati vikosi vya Tigray navyo vikielekea kwenye maeneo ya mipaka yake kwenye jimbo hilo.

Eritrea yatupilia mbali madai yaliyotolewa na Ethiopia

Kwa mujibu wa chanzo hicho, hali inayoshuhudiwa haioneshi dalili nzuri na ikiwa jumuiya ya kimataifa haitoweka shinikizo kwa pande zote mbili kwenye mzozo huu kutafuta suluhu kupitia mazungumzo, hatari ya kuzuka vita itaongezeka.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2020-2022  kati ya jeshi la Ethiopia likisaidiwa na Eritrea dhidi ya kundi la ukombozi wa Tigray TPLF viliua takriban watu 600,000 kwa mujibu wa Umoja wa Afrika.