1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAsia

Waliokufa kwa tetemeko la ardhi Indonesia wapindukia 260

Iddi Ssessanga
22 Novemba 2022

Waokoaji nchini Indonesia wanaendelea kutafuta manusura waliofukiwa chini ya vifusi baada ya tetemeko la ardhi lililopiga kisiwa kikuu cha Java kuuwa watu zaidi ya 260 na kuwajeruhi mamia kadhaa wengine.

https://p.dw.com/p/4Jt2E
Indonesien | Erdbeben in West-Java | BG
Picha: ADITYA AJI/AFP/Getty Images

Machumbulio, malori na vifaa vingine vizito vilivyotumwa usiku vimewasili katika mji ulioathirika zaidi wa Cianjur kusini mwa Jakarta. Mji huo ulioko katika mkoa wenye watu wengi zaidi nchini humo wa Java Magharibi, uko karibu na kitovu cha tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa 5.6 kwenye kipimo cha richter lililotokea Jumatatu mchana, ambalo liliwafanya wakaazi waliotishika sana kukimbilia hovyo mitaani, baadhi wakiwa wamefunikwa katika damu na vifusi.

Soma pia: Indonesia yaomba msaada wa dharura wa kimataifa

Awalia juhudi za uokozi zilikwamishwa na barabara zilizoharibiwa na madaraja, kukatika kwa umeme na ukosefu wa vifaa vizito. Hata hivyo ugavi wa umeme na mawasiliano ya simu vimeanza kuboreka katika maneo yaliokumbwa na tetemeko hilo siku ya Jumanne.

Indonesien | Erdbeben in West-Java | BG
Wanakijiji wakibeba wajeruhi kufuatia tetemeko la ardhi lililouwa watu zaidi ya 250.Picha: ADITYA AJI/AFP/Getty Images

Manusura mmoja aliejitambulisha kwa jina moja la Tartinem, amesema alihofia maisha ya familia yake. "Nilikuwa nalia na mara moja nikamshika mume wangu na watoto. Laiti kama nisingeliwavuta nje, tungegeuka wahanga. Nyumba ilikuwa inatikisika kama vile inacheza," alisema.

Wengi wa waliokufa walikuwa wanafunzi wa shule za umma waliokuwa wamefunga shule kwa siku hiyo na walikuwa wanachukuwa masomo ya ziada katika shule za Kiislamu wakati tetemeko lilipopiga, amesema gavana wa mkoa wa Java Magharibi Ridiwan Kamili, wakati akitangaza idadi mpya ya vifo katika eneo la mbali la vijijini.

Soma pia: Athari za Tsunami bado ni kubwa Indonesia

Mbali na waliouawa, mamlaka zimeripoti kuwa zaidi ya watu 300 waliumia vibaya na wasiopungua 600 wamepata majeraha madogo, lakini haikuwa wazi mara moja ni wangapi hawajulikani bado walipo.

Katika kijiji cha Cijedil, kaskazini-magharibi mwa Cianjur, tetemeko hilo lilisababisha mporomoko wa udongo na kuziba mitaa na kufukia nyumba kadhaa, na kulikuwa na ripoti kwamba watu 25 walikuwa bado wamefukiwa.

Indonesien | Erdbeben in West-Java | BG
Taswira ya uharibu uliosababishwa na tetemeko la ardhi mkaoni Java Magharibi, Indonesia.Picha: ADITYA AJI/AFP/Getty Images

Mamlaka ya hali ya hewa ya Indonesia imerikodi matukio yasipoungua 25 ya matetemeko madogo madogo yaliofuatia tetemeko hilo, huku gavana wa Java Magharibi akisema zaidi ya watu elfu 13 ambao nyumba zao zimeharibiwa vibaya walikuwa wanapelekwa kwenye vituo vya hifadhi.

Rais wa Indonesia Joko Widodo, ambaye amezuru kitovu cha tetemeko hilo leo, amesema serikali itatoa fidia kwa waathirika wa tetemeko hilo pamoja na familia zao.

Chanzo: mashirika