1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari za Tsunami bado ni kubwa Indonesia

Admin.WagnerD2 Oktoba 2018

Rais wa Indonesia Joko Widodo ameamuru waokoaji zaidi kupelekwa kwenye maeneo yalioathirika vibaya na tetemeko la ardhi pamoja na Tsunami ili kuongeza nguvu ya kutafuta wahanga zaidi wa janga hilo la kimaumbile.

https://p.dw.com/p/35rIv
Indonesien Das Roa-Roa Hotel auf Sulawesi nach dem Erdbeben
Picha: REUTERS

Rais Widodo ametoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumza na maafisa wa serikali wanaoratibu uokoaji kwenye kisiwa cha Sulawesi miongoni mwa vilivyoathiriwa vibaya na Tsunami na kutaka juhudi zaidi ziongezwe kwenye kuwatafuta na kuwaokoa wote ambao bado hawajapatikana.

Kadhalika Rais Widodo ameelekeza Wakala Mkuu wa Taifa wa uokoaji kutuma polisi na wanajeshi zaidi kwenye wilaya zilizoathiriwa zaidi na janga hilo ambazo baadhi zimepoteza miundombinu muhimu ikiwemo barabara na madaraja na njia muhimu kufunikwa na vifusi vya maporomoko ya udongo.

Kulingana na Wakala wa Uokozi wa Taifa idadi ya waliofariki hadi sasa imefikia 1,234 na wengine 799 wamejeruhiwa na wapo kwenye hali mahututi.

Wengi waliofariki ni kutoka mji mdogo wa Palu ulio kiasi kilomita 1500 ya mji mkuu Jakarta lakini maeneo mengine mengi bado hayajafikiwa tangu tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.5 katika kipimo cha Richter liliposababisha mawimbi ya Tsunami na kuipiga Indonesia Ijumaa iliyopita.

Juhudi za uokozi zinasusua

Indonesien Palu Massengrab für Tsunami-Opfer
Picha: DW/Nurdin Amir

Kusuasua kwa juhudi za uokozi kumezusha hasira kutoka kwa wakaazi wa maeneo yaliyoathiriwa na janga hilo ambao bado wanahangaika kupata msaada wa chakula na nishati na wamemtolea wito Rais Widodo kuchukua hatua za haraka kuwasaidia.

Serikali imeamuru misaada ya wahanga ipelekwe haraka kwa kutumia helikopta lakini kuna ishara ndogo ya kufika haraka hasa kwenye kisiwa cha Palu na walionusurika wamekata tamaa.

Shirika la Habari la Reuters limeripoti tukio moja la kuvamiwa na kuporwa kwa duka ambapo kiasi watu 100 walionekana wakipiga kelele na kugombania  bidhaa ikiwemo nguo, blangeti na maji ya kunywa.

Kuhusu mikasa ya aina hiyo inayoongezeka serikali imeitetea ikisema wahanga wanaweza kuchukua vitu muhimu na wamiliki wa maduka watalipwa baadaye.

Walioathiriwa wanapindukia milioni

Katika hatua nyingine Shirika la Msalaba Mwekundu limekadiria kuwa  zaidi ya watu milioni 1.6 wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi na Tsunami lililotajwa kuwa janga ambalo litazidi kuwa baya zaidi

Indonesien nach dem Erbeben und Tsunami in Palu l medizinische Versorgung
Picha: picture alliance/AP/T. Syuflana

Makamu wa Rais wa Indonesia Jusuf Kalla amesema idadi kamili ya watu waliouawa inaweza kupindukia maelfu.

Miili ya waliofariki bado imetapakaa  mitaani na waliojeruhiwa wanatibiwa kwenye mahema kwa sababu hospitali ziliharibiwa.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AP/APTN

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman