Wakaazi Turkana wataka kambi za Kakuma na Daadab zisifungwe | Matukio ya Afrika | DW | 08.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wakaazi Turkana wataka kambi za Kakuma na Daadab zisifungwe

Wakaazi wa Turkana nchini Kenya waitaka serikali ya Kenya kubatilisha msimamo wake wa kulitaka shirika linalowashugulikia wakimbizi UNHCR kuzifunga kambi za wakimbizi za Kakuma na Daadab.

Muda uliotolewa wa kufungwa kambi hizo umekamilika Alhamisi. Wakaazi wanahofia huenda ndoa zao zikavunjika iwapo wakimbizi watarejeshwa makwao kwani wengi wao wameoa au kuolewa na wakimbizi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma. 

Hali ya kawaida imeendelea kushuhudiwa katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma licha ya muda ulitolewa na serikali wa siku 14 kufungwa kwa kambi hiyo ambao umekamilika rasmi Alhamisi.

Biashara na maisha katika kambi yenyewe imeonekana kuendelea kama kawaida. Hata hivyo, wakaazi wa eneo hili ndiyo wameonekana kuingiwa na hofu kubwa wakati muda uliotolewa ukikaribia kukamilika.

Wiki mbili zilizopita,serikali kupitia wizara yake ya usalama wa ndani,ilitoa muda wa siku kumi na nne kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalowashugulikia wakimbizi UNHCR kuzifunga kambi ya Kakuma hapa jimboni Turkana na kambi ya Dadaab katika kaunti ya Garissa.

Tazama vidio 02:00

Mkakati wa kuwajengea wakimbizi nyumba za kudumu Kenya

Hatua hiyo imeendelea kuwapa wasiwasi wakaazi wa hapa Turkana wanaodai kuwa,endapo serikali itashinikiza kufungwa kwa kambi hizo,idadi kubwa ya wakaazi watasalia bila wake na waume kwani wengi wameoa kwenye kambi hizo na pia kuolewa na wakimbizi. Hawa ni baadhi ya wakaazi wa Kakuma wakielezea ghadhabu yao kwa serikali.

"Tumeoana nao,wao pia wameoa waturkana na kupata watoto wakenya halisi.Sasa watarudishwa wapi watu ambao wamekuwa wakenya?" amesema mmoja wa wakaazi.

Si hofu ya kusambaratika kwa ndoa tu,wakaazi pia wanahofia kuwa endapo kambi ya wakimbizi ya Kakuma itafungwa,athari katika sekta ya kibiashara itakuwa wazi na idadi kubwa ya biashara zitalazimika kufungwa kwa kukosa wateja na faida huku maelfu ya wengine wakikosa ajira.

"Wakimbizi wanafanya biashara hapa na uchumi wa Kakuma uko juu.Ukiangalia kwa umaakini,Kakuma na Kalokol ndizo hutoa ushuru mkubwa kwa serikali ya kaunti ya Turkana kwa hivyo wakiondoka,kiuchumi kutaenda chini,” amesema Mark.

Mbunge wa Turkana magharibi Daniel Epuyo anadai kuwa,viongozi kutoka eneo hili hawajahusishwa kwenye mpango huo wa serikali wa kutaka kuwaondoa wakimbizi kambini Kakuma.

Tazama vidio 00:55

Ziwa Turkana li hatarani - UNESCO

"Tulisikia tu kama tangazo na kwa hivyo,tunasubiri wakati tutaulizwa kutoa maoni yetu kwa sababu sisi kama wakaazi wa Turkana magharibi hatuna shida na wakimbizi ambao tumewahifadhi,” amesema Epuyo.

Kambi ya wakimbizi ya Kakuma ina jumla ya wakimbizi 206,458 kwa mujibu wa takwimu za serikali.

Hadi tunapoandaa taarifa hii,haijabainika iwapo serikali itahakikisha kambi hizo zinafungwa au itatoa muda zaidi wa majadiliano na mashirika husika.

Ifahamike kuwa,waziri wa usalama Fred Matiang'i alitangaza kwamba,hakuna majadiliano yatakayoandaliwa kuhusu uamuzi wa serikali wa kuzifunga kambi hizo.

Michael Kwena,DW Kakuma.