Wajerumani wawachagua viongozi wao leo | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 22.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Wajerumani wawachagua viongozi wao leo

Wajerumani wanapiga kura leo katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho wakati kansela wa sasa Angela Merkel akiwa na nafasi kubwa kabisa ya kushinda mhula wa tatu, ingawa yaweza kulazimika kuungana na mahasimu wake-

Wagombea wakuu katika uchaguzi wa mwaka huu; Peer Steibrück wa SPD na Angela Merkel wa CDU

Wagombea wakuu katika uchaguzi wa mwaka huu; Peer Steibrück wa SPD na Angela Merkel wa CDU

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kote nchini saa mbili za asubuhi huku karibu raia 62 milioni wakiwa na haki ya kupiga kura.

Baada ya kuuongoza uchumi mkubwa wa kwanza katika bara la Ulaya kupita katika msukosuko mkubwa wa madeni, Merkel amejitokeza kuwa maarufu zaidi kutokana na anavyotoa uhakika kama atoavyo mama kwa mtoto wake kwa viongozi ambao wameingia matatani kama vile nchini Ufaransa, Ugiriki, Italia na Uhispania.

Wachunguzi wa maoni ya umma wanaashiria kuwa wapiga kura watamchagua tena kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59, ambaye jina lake la utani , ni "Mutti", yaani mama anayeonekana kushabihiana zaidi na jina analotambulishwa nalo kila mara la mwanamke mwenye nguvu zaidi duniani.

Changamoto katika muundo wa serikali

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck akipiga kura yake leo

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck akipiga kura yake leo

Lakini suala muhimu hapa litakuwa nani ataunda serikali nae? "Ni mara chache hali imekuwa ya karibu hivyo. Muungano wa Merkel una wingi mdogo tu kwa mujibu wa maoni ya wapiga kura, limesema gazeti la Sueddeutsche Zeitung, na kuongeza kuwa wengi wa wapiga kura wapatao milioni 62 wanaamua katika dakika za mwisho nani wamuunge mkono.

Merkel anajigamba kuwa muungano wake wa sasa wa siasa za wastani za mrengo wa kulia umekuwa na mafanikio makubwa tangu baada ya Ujerumani mbili kuungana mwaka 1990, kwa kuwa na uchumi imara na kiwango cha chini cha ukosefu wa ajira ambacho kiko chini ya asilimia saba.

Lakini lengo alilojiwekea kwa ajili ya chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) kubaki madarakani na washirika wake wadogo katika serikali, chama kinachopendelea wafanyabiashara cha Free Democratis, FDP, linategemea majaaliwa ambayo hayana hakika kwa chama hicho kidogo. "Kuendelea kutawala pamoja na washirika wake wa sasa ni suala ambalo halina uhakika," Gero Neugebauer, mtaalamu wa masuala ya siasa kutoka chuo kikuu huria cha mjini Berlin amesema.

Ndoa isio na mapenzi kati ya CDU na SPD?

Iwapo muungano huo utashindwa kupata wingi wa kutosha kuweza kutawala, Merkel anaweza kulazimika kuingia katika mikono ya mahasimu wake wa jadi, chama cha Social Democratic , SPD, ambacho alikishirikisha katika kile kinachojulikana kama muungano mkuu, lakini usio na mapenzi, katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi.

Kura nyingi za maoni zinampa Bi Merkel nafasi kubwa ya kushinda

Kura nyingi za maoni zinampa Bi Merkel nafasi kubwa ya kushinda

Huku washirika wake wa Ulaya wakikodolea macho, chama kinachopinga muungano wa Ulaya , chama chaguo mbadala kwa Ujerumani, The Alternative for Germany, (AfD) kinaweza pia kupata mafanikio, ama kwa kuvutia kura za kutosha kuingiza wabunge katika bunge la Ujerumani ama kwa kuzipoteza kura za wapiga kura wa siasa za wastani za mrengo wa kulia.

"Kwa kansela Merkel chama hicho kisichopendelea muungano wa Ulaya kinakuwa tatizo," limesema gazeti la Spiegel mtandaoni katika mkesha wa uchaguzi. "Iwapo chama hicho kinachopinga Umoja wa Ulaya kitafaulu kuvuka kizingiti cha asilimia tano na kuingia bungeni , hali hiyo itaugharimu mno muungano wa njano na nyeusi yaani vyama tawala vya sasa vya CDU,CSU na FDP," limeongeza gazeti hilo.

Chaguzi tatu za kabla ya uchaguzi huu, zimeonesha kuwa chama cha AfD, ambacho kinataka kuachana na sarafu ya euro na kuvunjwa kwa muungano wa mataifa ya eneo la euro, kimeshindwa kuvuka kiunzi cha asilimia tano zinazotakiwa kwa chama kuingia katika bunge.

Kwa hiyo swali kubwa ni, chama gani ambacho Bibi Merkel atashirikiana nacho kuunda serikali ya mseto.

Muungano wake wa sasa unaonekana kuwa na ushindi mdogo kulingana na utafiti wa maoni ya wapiga kura, ambao wengi wao huamua dakika ya mwisho.

Matokeo ya awali yataanza kufahamika saa 12 za jioni mara tu baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa,afp

Mhariri: Daniel Gakuba

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com