Wafuasi wa Mursi wakiuka agizo la serikali na kuandamana | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wafuasi wa Mursi wakiuka agizo la serikali na kuandamana

Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani nchini Misri Mohammed Mursi wamefanya maandamano makubwa Ijumaa jioni(02.08.2013) na kukabiliana na polisi mjini Cairo baada ya serikali kuagiza kambi zao kuvunjiliwa mbali

Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya kiasi ya waandamanaji 1,000 waliojaribu kukita kambi mpya nje ya uwanja mkubwa uliotengewa vituo vya habari.

Makabiliano hayo yalizuka huku naibu waziri wa mambo ya nje ya Marekani William Burns akiwasili mjini Cairo akiwa miongoni mwa maafisa wa ngazi ya juu wa kimataifa kuwasili nchini humo kujaribu kuwashurutisha wafuasi wa Mursi na serikali kukaa katika meza ya mazungumzo ili kutatua mzozo uliopo.

Wakati huo huo, mkuu wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda Ayman al Zawahiri ambaye ni mzaliwa wa Misri ameishutumu Marekani kwa kile alichokitaja kufanya njama ya kuipindua serikali ya Mursi wakishirikiana na jeshi na jamii ya kikristo nchini humo walio wachache.

Mkuu wa mtandao wa kigaidi Al Qaeda Ayman al-Zawahiri

Mkuu wa mtandao wa kigaidi Al Qaeda Ayman al-Zawahiri

Mkuu wa Al Qaeda azungumzia mzozo wa Misri

Katika matamshi yake ya kwanza tangu mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 3 mwezi uliopita,Zawahiri pia aliushutumu upande wa upinzani wenye nadharia zinazopinga dini kuwa msingi wa maadili na wakristo wa dhehebu la Coptic ambao alisema wanataka kujitenga na kuunda serikali yao na kutaka kuwe na maandamano makubwa ya kurejesha sheria za Kiislamu.

Mjini Cairo,wafuasi wa Mursi walimiminika mabarabarani baada ya sala ya Ijumaa.Waandamanaji hao wamesimama kidete na azma yao ya kuandamana hadi Mursi arejeshwe madarakani licha ya ukandamizaji na vitisho kutoka kwa jeshi na asasi za kiusalama dhidi yao.

Wizara ya mambo ya ndani imewahimiza wale waliokita kambi katika eneo la Rabaa al Adawiya na Nahda kuruhusu hekima na maslahi ya kitaifa kutawala na kuondoka mara moja kutoka maeneo hayo.Gazeti la serikali la Al Ahram liliripoti hapo jana kuwa polisi ina mipango ya kuwatawanya waandamanaji hao lakini wanatafuta njia ya amani kufanya hivyo.

Makamu wa rais wa Misri Mohammed El Baradei ametoa wito wa kusitishwa kwa ghasia na kuongeza kuwa punde tu baada ya kusitishwa kwa machafuko hayo;watashiriki katika mazungumo ili kuhakikisha udugu wa kiislamu unaelewa kuwa Mursi alishindwa na hiyo haimaanishi kuwa kundi hilo litatengwa kwa namna yoyote.

Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani William Burns amewasili Mjini Cairo

Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani William Burns amewasili Mjini Cairo

Zaidi ya watu 250 wameuawa tangu Mursi kuondolewa madarakani na juhudi za kidiplomasia za kuzuia umwagikaji zaidi wa damu zimeshika kasi.

Burns aliwasili Cairo jana jioni(02.08.2013) siku chache tu baada ya mjumbe wa umoja wa Ulaya kuhusu mashariki ya kati Bernardino Leon, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na mkuu wa sera za kigeni Bi Catherine Ashton pia kwenda Misri kukutana na viongozi wa pande zote mbili.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Sekione Kitojo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com