Wafaransa wanamchaguwa rais mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wafaransa wanamchaguwa rais mpya

Wafaransa Jumapili (07.05.2017) wanamchaguwa rais mpya kati ya Emmanuel Macron wa sera za wastani na kiongozi wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen uchaguzi muhimu kwa mustakbali wa nchi hiyo na Ulaya.

 

Wapiga kura nchini Ufaransa Jumapili (07.05.2017) wanamchaguwa rais mpya kati ya mgombea wa kujitegemea wa sera za mrengo wa kati Emmanuel Macron na kiongozi wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen katika uchaguzi muhimu kwa mustakbali wa nchi hiyo na Ulaya.

Uchaguzi huu unafuatia kampeni kali za kushutumiana, kashfa, mambo ya maajabu na shambulio la udukuzi la dakika za mwisho dhidi ya Macron mtaalamu wa zamani wa benki ya uwekezaji mwenye umri wa miaka 39 ambaye hakuwahi kushika madaraka kwa kuchaguliwa na wananchi.

Marudio hayo ya uchaguzi yanawapambanisha Macron mwenye kupendelea biashara na Umoja wa Ulaya na Le Pen mwenye kupinga wahamiaji na Umoja wa Ulaya, dira mbili tofauti kabisa zinazoonyesha mgawiko katika demokrasia ya mataifa ya uliwengu wa magharibi.

Le Pen mwenye umri wa miaka 48 ameuelezea uchaguzi huo kuwa ni pambano kati ya "watandawazi " wanaowakilishwa na mpinzani wake  ambao wanapendelea biashara huru, wahamiaji na kushirikiana utaifa dhidi ya " wazalendo " ambao wanatetea kuwepo kwa ulinzi madhubuti mipakani na utambulisho wa kitaifa.

Matokeo yatashangaza ?

Frankreich Präsidentschaftswahl Marine Le Pen (picture-alliance/dpa/O. Corsan)

Marine Le Pen kiongozi wa sera kali za mrengo wa kulia akipiga kura yake.

Le Pen anataraji kupata matokeo ya kushangaza ambayo yatahanikiza kama vile uamuzi wa Uingereza kujitowa kwenye Umoja wa Ulaya au ushindi wa Rais Donald Trump wa Marekani ambao ulikuwa haukutarajiwa.

Le Pen amepiga kura yake katika ngome yake kuu ya Henin-Beaumont kaskazini mwa nchi hiyo ambapo wanaharakati wa kike wakiwa vifua wazi waliparamia jukwaa la kanisa na kuonyesha bango lenye kusomeka "Mdaraka kwa Marine, kata tamaa kwa Marianne" likikisudia alama ya Ufaransa.

Macron alipiga kura yake katika mji wa kitalii wa Torque ulioko kwenye fukwe za kaskazini mwa nchi ambapo ana nyumba ya mapumziko.

Rais anayeondoka madarakani Francois Hollande ambaye hapo mwezi wa Disemba aliamuwa kutowania kuchaguliwa tena alipiga kura katika jimbo lake la uchaguzi la zamani la Tulle katikati ya Ufaransa.Hollande ambaye alimtoa Macron kutoka mtu asiefahamika kabisa na kumteua kuwa waziri wa uchumi hapo mwaka 2014 amesema daima kitendo cha kupiga kura ni muhimu kabisa kikiandamana  na matokeo mazito."

Kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura

Frankreich Präsidentschaftswahl in Marseille (picture-alliance/AP Photo/C. Paris)

Wapiga kura mjini Marseille.

Kufikia mchana idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa asilimia 28.2 ikiwa chini kutoka asilimia 30.7 ilioshuhudiwa wakati huo huo katika uchaguzi wa mwisho wa rais hapo mwaka 2012.

Takriban vituo vyote vya kupiga kura vinafungwa saa moja lakini vile vilioko katika miji mikubwa vitabakia wazi kwa saa moja zaidi. Makadirio ya kwanza ya matokeo yatatangazwa saa tatu.

Uchunguzi wa mwisho wa maoni  umeonyesha Macron ambaye alishinda duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi uliopita alikuwa akiongoza kwa asilimia 62 dhidi ya 38 za Le Pen kabla ya kufichuliwa kwa taarifa za udukuzi hapo Ijumaa jioni. Mara moja amri ya kutotangazwa kwa habari hizo ilitekelezwa muda mfupi baada ya hapo.

Mamia kwa maelfu ya baruwa pepe na nyaraka ziliibiwa kutoka kitengo cha kampeni cha Macron na kutupwa mtandaoni na baadae kusambazwa na kundi la mtandao lenye kupinga siri la Wikileaks kwa kile Macron alichokiita kuwa ni "kuyumbisha demokrasia."

Mamlaka ya uchaguzi nchini Ufaransa ilisema kuchapisha nyaraka hizo linaweza kuwa kosa la jinai onyo ambalo limezingatiwa na vyombo vikuu vya habari na kukiukwa na wapinzani wa Macron na wanaharakati wa sera kali za mrengo wa kulia mtandaoni.

Usalama waimarishwa

Frankreich Präsidentschaftswahl in Paris Sicherheitskräfte (DW/B. Riegert)

Uwa wa makumbusho ya Louvre mjini Paris.

Uwa wa makumbusho ya Louvre mjini Paris ambapo Macron anatarajiwa kuzungumza baadae usiku watu waliondolewa kwa muda mfupi baada ya kugundulikana kwa begi lililokuwa likitiliwa mashaka.

Polisi katika mji mkuu huo wa Ufaransa imesema imefanya ukaguzi wa usalama katika eneo hilo kwa ajili ya kuchukuwa tahadhari na baadae imeongeza kusema hali imerudia kuwa ya kawaida katika eneo hilo.

Kwa yoyote yule atakayeshinda uchagauzi huo anatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa Ufaransa nchi ambayo uchumi wake unashikilia nafasi ya sita kwa kuwa na nguvu kubwa duniani, mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taifa lenye nguvu kubwa za kijeshi duniani.

 

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP /Reuters

Mhariri : Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com