1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiEritrea

Waeritrea wapitia mateso katika zoezi la huduma ya kitaifa

8 Agosti 2023

Mpelelezi huru wa UN amesema wakimbizi wa Eritrea wameeleza kupitia mateso, unyanyasaji wa kingono, kulazimishwa kufanya kazi ngumu na kuwekwa katika mazingira ya kikatili wakati wa zoezi la lazima la huduma ya kitaifa.

https://p.dw.com/p/4UtYX
Äthiopien | Sexuelle Gewalt
Mhanga wa unyanyasaji wa kingono Picha: privat

Mpelelezi huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Mohamed Babiker amesema katika ripoti iliyotolewa jana Jumatatu kuwa wakimbizi wa Eritrea na waomba hifadhi wameeleza kwamba wamepitia mateso, unyanyasaji wa kingono na kijinsia, kulazimishwa kufanya kazi ngumu na kuwekwa katika mazingira ya kikatili wakati wa zoezi la lazima la huduma ya kitaifa ambalo aghalabu hutoa mafunzo ya msingi ya kijeshi. 

Mohamed Babiker amesema Eritrea ina sera ya lazima kulihudumia taifa kwa muda usiojulikana, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya utumishi kwa umma na mafunzo ya kijeshi.

Soma pia: Wanajeshi wa Eritrea waondoka Tigray

Mpelelezi huyo huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu ameeleza kuwa serikali ya Eritrea imepuuza miito kadhaa kutoka mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kuhakikisha uwepo wa ukomo wa huduma hizo za kitaifa na pia kulinda haki za binadamu za washiriki wote.

Hata hivyo, Eritrea imeshikilia msimamo wake kuwa mpango wake wa huduma ya kitaifa umepewa "sura tofauti” na baadhi ya mashirika ya kigeni.

Licha ya hoja zinazotolewa na Eritrea kuutetea mpango wake huo wa huduma ya kitaifa, Babiker ameongeza kuwa anaendelea kupokea ripoti nyingi na za kuaminika juu ya visa vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika muktadha wa watu kulazimishwa kujiunga na mafunzo ya kijeshi.

Babiker ameeleza kuwa watu hawana hiari ya kuchagua iwapo wangependa kujiunga na huduma hiyo ya kitaifa au la na kwamba wanaokwepa, wanakabiliwa na mkono mrefu wa serikali ikiwemo kuwekwa kizuizini, kutoweka kusikojulikana na kuteswa.

Eritrea yashtumiwa kwa kubinya uhuru wa kujieleza

Isaias Afwerki
Rais wa Eritrea Isaias Afwerki akizungumza katika mkutano na wanahabari mjini NairobiPicha: Khalil Senosi/AP Photo/picture alliance

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameielezea Eritrea kama mojawapo ya mataifa kandamizi duniani na yenye kubinya uhuru wa watu wake. Tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ethiopia miongo mitatu iliyopita, taifa hilo dogo la Pembe ya Afrika limekuwa chini ya uongozi wa Rais Isaias Afwerki, ambaye hajawahi kufanya uchaguzi.

Babiker amesema Rais Afwerki amekataa kuiheshimu katiba ya mwaka 1997 na kwamba anaiongoza nchi hiyo bila ya utawala wa kisheria. 

Soma pia: Marekani yaiwekea vikwazo Ethiopia na Eritrea

Mpelelezi huyo maalum wa Umoja wa Mataifa amesema mahojiano aliyoyafanya na waomba hifadhi na wakimbizi huko Eritrea, yanaweka wazi kuwa ulazima wa watu kujiunga na huduma ya kitaifa ni moja ya sababu kuu za watu kuikimbia nchi hiyo.

Amesema katika ripoti yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayojumlisha hali ya mambo nchini Ertitrea katika kipindi cha miezi 12 hadi Aprili 24, "mpango wa huduma ya kitaifa, ambao umewekwa kwa lengo la maendeleo ya taifa, japo kwa vitendo unadhoofisha ukuaji wa taifa kwa kuwalazimisha vijana kuikimbia Eritrea.”

Vyombo vya habari vya Sweden vimeripoti kuwa ripoti hiyo ilisambazwa siku chache baada ya tamasha la utamaduni la Eritrea lililokuwa linafanyika katika kitongoji cha Järvafältet kaskazini mwa mji mkuu wa Sweden wa Stockholm kugeuka na kuwa la vurugu baada ya maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali ya Eritrea kuvamia tamasha hilo, na kusababisha majeruhi ya watu 52.

Sweden imewapa hifadhi maelfu ya watu wenye asili ya Eritrea.