1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waathiriwa wa shambulio la Gatumba bado wanadai haki

Amina Mjahid Iddi Ssessanga
14 Agosti 2019

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limesema waathirika wa shambulio katika kambi moja ya wakimbizi Burundi pamoja na familia zao, bado wanasubiri haki na fidia miaka 15 baada ya tukio hilo.

https://p.dw.com/p/3NsX6
Massenbeerdigung in Gatumba
Picha: picture-alliance/AP Photo

Shambulio hilo lililotokea katika kambi ya wakimbizi ya Gatumba lilisababisha mauaji ya watu 150 raia wa Congo na kuwajeruhi wengine 106.

Kesi ya uhalifu ilifunguliwa mwaka 2013 lakini ikakwama mwaka 2014 na haijaendelea tena tangu wakati huo. Kulingana na Lewis Mudge Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch upande wa Afrika ya kati, serikali ya Burundi inapaswa kuhakikisha mahakama inabakia huru kutoingiliwa na siasa na kuhakikisha kuwa haki inapatikana kulingana na sheria ya Burundi na ya kimataifa.

Bujumbura Burundi Protest Gewalt
Moja wa maafisa wa polisi nchini Burundi Picha: picture-alliance/D. Kurokawa

"Serikali inawajibika kuhakikisha haki inapatikana kwa waathiriwa pamoja na familia zao, kuacha kuwalinda wakosaji kutasaidia kufunga vidonda vya wale wanaoteseka na waathiriwa wa shambulio hilo na pia itaonesha kwamba suala la uwajibikaji linachukuliwa kwa umakini nchini Burundi." alisema  Lewis Mudge.

Mnamo Agosti 13, mwaka 2004, wanachama wa chama cha ukombozi wa kitaifa  National Forces of Liberation FNL waliwashambulia wakimbizi hasa wa jamii ya Banyamulenge ambao ni watutsi wanaotokea mkoa wa Kivu katika Jamhuri ya kidemokrasi ya congo katika shambulio hilo la kikabila.

FNL vuguvugu la wahutu wanaotokea Burundi waliwapiga risasi na kuwachoma wakimbizi hao wa kutokea Congo huku wakimbizi wengine kutoka makabila mengine wakinusurika pamoja na raia wa Burundi wanaoishi katika sehemu nyengine ya kambi hiyo ya Gatumba.

Shirika la Human Rights Watch limegundua kuwa maafisa wa kijeshi na polisi wa Burundi wakati huo walikosa kuuuingilia mkasa huo licha ya kwamba mauaji yalitokea mita chache kutoka katika kambi yao.

Baadhi ya waathirika wasema kamwe hawatoweza kusahau kilichotokea

Muathirika mmoja aliyenusurika kifo katika shambulio hilo la Gatumba aliliambiwa shirika la human rights watch kuwa anakumbuka kilichotokea, alikuwa na miaka 11 lakini uchungu wa kumuona mtu akiungua hadi kukata roho ni kitu asichoweza kukisahau.

Hata hivyo muda mfupi baada ya shambulio hilo kundi la FNL lilikiri kuhusika, na miaka kadhaa baadaye msemaji wake wakati huo Pasteur Habimana amekanusha kutoa taarifa kama hiyo.

Tansania Flüchtlinge aus Burundi Cholera
Baadhi ya wakimbizi nchini BurundiPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Kundi hilo lilikubali kuweka silaha chini na kuwa chama cha kisiasa mwaka 2009 hatua iliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Mmoja wa wanachama wake ambaye serikali ya burundi ilitoa ilani ya kumatwa kwakwe  mwaka 2004 ni Agathon Rwasa ambaye anabakia kuwa kiongozi muhimu wa upinzani. Rwasa hakuwahi kukamatwa kufuatia msamaha aliyoupata kutokana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini mwaka 2006.

Kwa sasa shirika la Human Rights Watch linasema Burundi inapaswa kuchukua hatua, kuhakikisha waliyohusika na shambulio la Gatumba wanakabiliwa na mkono wa sheria na kutambua haki ni muhimu katika kuzuwiya ukatili zaidi. 

Chanzo:Human Rights Watch