1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wajitenga na mapatano ya kusitisha mapigano

Iddi Ssessanga
25 Novemba 2022

Kundi la waasi la M23 limesema mapatano ya usitishaji mapigano yaliotangazwa Jumatatu hayalihusu, huku likitoa wito wa mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

https://p.dw.com/p/4K2yh
DR Kongo M23-Rebellen,
Picha: Joseph Kay/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa kisiasa wa kundi hilo Lawrence Kanyuka ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kuwa M23 ilionya waraka wa mapatano hayo kupitia mitandao ya kijamii, na kwamba hakukuwa na mwakilishi wao kwenye mkutano mdogo wa kilele uliofikia maamuzi hayo, hivyo tangazi hilo haliwahusu.

Aliongeza kuwa kawaida panapokuwa na usitishaji mapigano, makubaliano yake huwa kati ya pande mbili zinazopambana.

Wataalamu waionya Congo kuwajumuisha waasi jeshini

Rais wa DRC Felix Tshisekedi na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta, walihudhuria mkutano huo uliofanyika katika mji mkuu wa Angola, Luanda siku ya Jumatano.

Kwenye mkutano wa waandishi habari mjini Kinshasa siku ya Alhamisi, waziri wa mambo ya nje wa Congo, Christophe Lutundula, alisema leo saa 12 kamili jioni M23 wanapaswa kusitisha mashambulizi yao yote.Kanyuka alisema waasi walitangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja mnamo mwezi Aprili, na anaamini mpango huo ulikuwa unaendelea bado, akisisitiza kuwa endapo serikali haitawashambulia Ijumaa saa 12 jioni au asubuhi, wataendelea kuwepo pale, vinginevyo wanajitetea tu.DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC

Wakaazi wakimbia machafuko yanayofanywa na waasi wa M23 wanaokabiliana na vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mashariki mwa Congo.
Wakaazi wakimbia machafuko yanayofanywa na waasi wa M23 wanaokabiliana na vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mashariki mwa Congo.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Msemaji huyo wa M23 alisema wao wako tayari wakati kufanya majadiliano ya moja kwa moja na serikali ili kutatua mzizi wa mizozo.

Serikali mjini Kinshasa hata hivyo imekataa kushirika mazungumzo na kundi la M23, ambalo inaliita vuguvugu la kigaidi, maadamu linaendelea kukalia maeneo nchini DRC.

Mwanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akishika doria karibu na helikopta baada y amakabiliano na waasi wa M23 eneo la Rutshuru, umbali wa kilomita 70 kutoka Goma.
Mwanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akishika doria karibu na helikopta baada y amakabiliano na waasi wa M23 eneo la Rutshuru, umbali wa kilomita 70 kutoka Goma.Picha: Guerchom Ndebo/AFP/Getty Images

Kundi la M23 limekuwa bwete kwa miaka kadhaa, lakini lilichukuwa tena silaha mwaka jana na limetazamwa tangia mwanzo na serikali ya Congo kama linaloungwa mkono na Rwanda, ambayo hata hivyo inakanusha madai hayo.

Waasi hao hivi karibuni waliteka maeneo makubwa ya kaskazini mwa mji wa Goma, ambao ndiyo mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kenyatta azuru mji wa Goma katikati mwa mzozo wa waasi

Mkutano wa kilele wa Luanda ulihitimishwa kwa makubaliano ya kusitisha uhasama mashariki mwa Congo kuanzia Ijumaa jioni, ukifuatia na kuondoka kwa M23 kutoka maeneo inayoyakalia na kurejea kwenye maeneo yao ya awali.

Endapo waasi hao watakaidi agizo hilo, kikosi cha kikanda cha Afrika Mashariki kinachopelekwa mjini Goma kitawafurusha nje, yalisema makubaliano hayo.