1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji walivamia bunge Iraq

28 Julai 2022

Mamia ya wafuasi wa kiongozi wa kidini wa Iraq Moqtada al-Sadr walilivamia bunge Jumatano ambapo walionekana wakiimba na kucheza baada ya kuwazidi nguvu maafisa wa usalama.

https://p.dw.com/p/4ElK0
Irak I Anti-Korruptions-Proteste in Bagdad
Picha: Ahmed Saad/REUTERS

Waandamanaji hao walikuwa wanapinga uteuzi wa Mohammed al-Sudani kama mtu aliyeteuliwa rasmi na muungano unaoongozwa na vyama vya Kishia vinavyoungwa mkono na Iran na marafiki zao.

Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi katika harakati za kuwazuia waandamanaji hao wasivunje lango ila waliwazidi nguvu na kuingia bungeni.

Waandamanaji hao ambao wote walikuwa wanaume, walionekana wakitembea katika meza za bunge, wakipekua pekua madaftari bungeni humo na wengine walionekana wakiwa wameketi katika viti vya wabunge wakipeperusha bendera za Iraq.

Waondoka bungeni baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa kiongozi wao

Hakuna wabunge waliokuwa bungeni wakati wa tukio hilo, ni maafisa wa usalama tu ila walionekana kuwa watulivu na kuwakubalia waandamanaji hao wafanya wanachotaka.

Irak I Anti-Korruptions-Proteste in Bagdad
Waandamanaji wakiimba na kucheza ndani ya bunge la IraqPicha: Ahmed Saad/REUTERS

Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhemi alitoa wito kwa waandamanaji hao kuondoka mara moja bungeni akiwaonya kwamba maafisa wa usalama watahakikisha kulindwa kwa taasisi na kuzuia vurugu zozote. Waandamanaji hao lakini hawakuonekana kubabaishwa na ujumbe wa waziri huyo mkuu.

Saa chache baadae al-Sadr aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akiwaambia wafuasi wake kwamba ujumbe wao umepokelewa na kuwaamuru kurudi majumbani kwao. Muda mfupi baadae, waandamanaji hao walianza kuondoka bungeni humo huku maafisa wa usalama wakiwatazama kwa karibu.

Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa pia kuhusiana na maandamano hayo ukisema Wairaqi wana haki ya kuandamana ila maandamano hayo yanastahili kuwa yenye utulivu na yanayofuata sheria.

Al-Sadr awashinikiza wabunge wajiuzulu

Haya ndiyo yaliyokuwa maandamano makubwa zaidi tangu kufanyika kwa uchaguzi mwezi Oktoba na pia hii ilikuwa mara ya pili al-Sadr kutumia ushawishi wake kuwakusanya wafuasi wake na kutuma ujumbe kwa mahasimu wake wa kisiasa mwezi huu.

Irak Muktada al Sadr
Kiongozi wa kidini mwenye ushawishi Moqtada al-SadrPicha: Ali Najafi/AFP/Getty Images

Muungano wa al-Sadr ulishinda viti 73 katika uchaguzi wa mwaka uliopita, ushindi ulioufanya kuwa muungano mkubwa katika bunge la Iraq lenye wabunge 329. Ila tangu kura hiyo, mazungumzo ya kuunda serikali yamekwama.

Awali Sadr alikuwa anaunga mkono wazo la serikali ya wengi, hatua ambayo ingewasukuma wapinzani wake wa Kishia katika upinzani. Lakini kiongozi wa kijeshi wa zamani aliwashangaza wengi kwa kuwalazimisha wabunge wake wajiuzulu, hatua iliyoonekana kama ya kuwashinikiza mahasimu wake waunde serikali.

Wabunge wapya 64 waliapishwa mnamo mwezi Juni na kuufanya muungano huo unaoungw amkono na Iran kuwa muungano mkubwa zaidi bungeni.