1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIraq

Waziri Mkuu wa Iraq anusurika jaribio la mauaji

Mohammed Khelef
7 Novemba 2021

Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Khadhimi, amenusurika jaribio la mauaji lililofanywa kwa kutumia ndege zisizo rubani zenye silaha zilizoyalenga makaazi yake katika Ukanda wa Kijani wenye ulinzi mkali mjini Baghdad.

https://p.dw.com/p/42gPn
Irak Ministerpräsident Mustafa Al Khadhimi
Picha: AFP/Prime Minister's Media Office

Maafisa wa serikali yake wanasema Khadhimi hakudhurika kutokana na mashambulizi hayo yaliyofanika mapema siku ya Jumapili (Novemba 7). 

Mashambulizi hayo ni ishara ya hali kuelekea kubaya zaidi iliyochochewa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kukataa kuyatambuwa matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa mwezi uliopita.

Maafisa wawili wa serikali ya Iraq waliliambia shirika la habari la AP kwamba walinzi saba wa Khadhimi walijeruhiwa kwa mashambulizi ya ndege mbili zenye silaha zisizo rubani, yaliyotokea kwenye eneo mashuhuri la Ukanda wa Kijani, ambalo kawaida linakuwa na ulinzi mkali.

"Maroketi ya mahaini hayatatuondosha hata hatua moja kwenye msimamo wetu na dhamira ya walinzi wetu mashujaa," Khadhimi aliandika kwenye ukurasa wa Twitter muda mfupi baada ya mashambuli hayo. "Niko salama na nipo baina ya watu watu. Alhamdulillah!"

Mashambulizi kwenye Ukingo wa Kijani

Irak Bagdad | Protest gegen Wahlergebnis und Ausschreitungen
Maandamano dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge nchini Iraq katika eneo liitwalo Ukanda wa Kijani.Picha: Wisam Zeyad Mohammed/Anadolu Agency/picture alliance

Kwenye taarifa yake, serikali ilisema ndege hizo zisizo rubani zilijaribu kuishambulia nyumba ya Khadhimi.

Wakaazi wa Baghdad walisikia sauti za mripuko kufuatia milio ya risasi kutokea upande wa Ukanda wa Kijani, ambao una majengo mengi ya ofisi za kibalozi na ofisi za serikali.

Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali ilisema jaribio hilo lililoshindwa la mauaji lilifanyika "kwa ndege yenye miripuko ambayo ilijaribu kuyapiga makaazi ya waziri mkuu katika Ukanda wa Kijani."

"Vyombo vya usalama vinachukuwa hatua zinazohitajika kuhusiana na umuhimu na jaribio hili lililoshindwa," ilisema taarifa hiyo.

Haikufahamika mara moja aliyehusika na mashambulizi hayo wala hakukuwa na aliyebeba dhamana yake, lakini yametokea wakati kukiwa na mkwamo baina ya vikosi vya usalama na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, ambao wafuasi wao wamepiga kambi nje ya Ukanda wa Kijani kwa takribani mwezi mzima baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa bunge, ambao walishindwa vibaya.

"Jaribio hili la mauaji ni kiwango cha juu cha kuzorota kwa hali, yakivuuka mpaka katika njia isiyotegemewa ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya kabisa," aliandika Ranj Alaadin, mtaalamu wa Taasisi ya Brookings katika ukurasa wa Twitter.

Mzozo wa uchaguzi waendelea

Irak Anti Regierungsproteste Mustafa al-Kadhemi
Wafuasi wa makundi ya Kishia wakichoma moto picha za Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi, wanayemlaumu kwa matokeo ya uchaguzi wa bunge wa mwezi Oktoba 2021.Picha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Maandamano ya siku ya Ijumaa (Novemba 5) yaligeuka mauaji baada ya waandamanaji kuelekea Ukanda huo wa Kijani, kulipotokea urushianaji risasi na mmoja kati ya waandamanaji wa upande wa wanamgambo kuuawa na walinzi kadhaa wa upande wa serikali kujeruhiwa.

Khadhimi aliamuru uchunguzi kujuwa chanzo cha mapigano hayo na kumtambuwa aliyekaidi amri ya kutokurusha risasi.

Baadhi ya viongozi wa makundi ya wanamgambo yenye nguvu na yaliyo na utiifu kwa Iran yalimtuhumu Khadhimi kwa mapigano ya Ijumaa na kifo cha mwandamanaji huyo.

"Damu ya shahidi huyu itakuwajibisha," alisema Qais al-Khazali, kiongozi wa wanamgamo wa Asaib Ahl al-Haq, akimkusudia Kadhimi kwenye maziko ya mwandamanaji huyo aliyeuawa.