Waafrika wanaoshtakiwa ICC | Matukio ya Afrika | DW | 06.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waafrika wanaoshtakiwa ICC

Waafrika 24 hivi sasa wanakabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilioko The Hague nchini Uholanzi. Hukumu moja tayari imetolewa lakini wengi wa washtakiwa bado hawakufikishwa mahakamani kwenyewe.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague Uholanzi.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague Uholanzi.

Ivory Coast

Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo.

Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo.

Laurent Gbagbo : Rais wa zamani wa Ivory Coast yuko mahabusu mjini The Hague tokea mwezi wa Novemba mwaka 2011.Hata hivyo mahakama imesema hadi sasa hakuna ushahidi wa kutosha dhidi yake kuyakinisha kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinaadamu wakati wa machafuko yaliozuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 nchini Ivory Coast.Mashtaka didi yake yanamtuhumu kwa kuhusika na mauaji ya takriban watu 166,ubakaji,dhuluma na ukandamizaji wa wapinzani wake wa kisiasa.

Mashtaka kama hayo yanamkabili mke wa rais Simone Gbagbo na waziri wa zamani wa vijana Charles Ble Goude.Wote wawili wako kizuizini nchini mwao ambapo hivi sasa inajadiliwa iwapo waachiliwe chini ya sera ya usuluhishi ya taifa.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

Thomas Lubanga akisikiliza hukumu ya kesi yake mjini The Hague tarehe 10 Julai 2012.

Thomas Lubanga akisikiliza hukumu ya kesi yake mjini The Hague tarehe 10 Julai 2012.

Thomas Lubanga Dyilo : kiongozi wa zamani wa waasi wa Vikosi vya Kizalendo vya Ukombozi wa Congo (FPLC) ni mtu pekee hadi sasa aliyepatikana na hatia katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na hivi sasa yuko kwenye gereza la Schveningen karibu na The Hague.Alihukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani hapo mwezi wa Machi mwaka 2012 kwa kuwaandikisha askari watoto mashariki ya Congo.

Germain Katanga : Akiwa kama kiongozi wa kundi la Upinzani la Kizalendo la (FRPI) huko Ituri anashtakiwa kwa kuhusika huko Katanga kwa mauaji makubwa ya mashariki ya Congo hapo mwezi wa Februari mwaka 2003.Kesi yake imeahirishwa hadi mwezi wa Machi.

Mathieu Ngudjolo : Kiongozi wa kundi la Muungano wa Kitaifa la (FNL) mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokorasi ya Congo ni mshtakiwa mwenza katika kesi ya Katanga lakini aliachiliwa huru hapo mwezi wa Disemba mwaka 2012 kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Bosco Ntaganda : Kiongozi wa kundi la wanamgambo la Ulinzi wa Taifa wa Wananchi (CNDP) yuko kizuizini tokea mwaka 2013 baada ya kujisalimisha mwenyewe huko The Hague.Anashtakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu katika mzozo wa jimbo la Ituri. Baadae akiwa kama kamanda wa kundi la waasi la M23 alieneza hofu na vitisho mashariki ya Congo.Kesi dhidi yake inatarajiwa kuanza kusikilizwa hapo mwezi wa Februari mwaka 2014.

Sylvestre Maudacumura : Anayedaiwa kuwa kamanda wa kundi la Vikosi vya Demokrasia vya Ukombozi wa Rwanda(FDLR) anakabiliwa na makosa manane ya uhalifu wa kivita ukiwemo ubakaji, utesaji na mauaji.

Kenya

Machafuko ya baada ya uchaguzi Kenya 2007-2008.

Machafuko ya baada ya uchaguzi Kenya 2007-2008.

Uhuru Muigai Kenyatta

Rais wa sasa wa Kenya anatuhumiwa kwa kutowa ushirikiano wake katika uhalifu dhidi ya ubinaadamu wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008.Mchakato wa kesi yake umeanza tarehe nne mwezi wa Februari mwaka 2014.

Makamo wa Rais wa Kenya William Samoei Ruto na mtangazaji wa radio Joshua Arap Sang wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, kuhamisha watu na ukandamizaji.Mchakato wa kesi hiyo umekuwa ukisikilizwa tokea mwezi wa Septemba mwaka 2013.Ruto hivi sasa analazimika kushiriki kwenye kesi hiyo kwa kupitia kiungo cha mawasiliano ya video kutoka Kenya.

Walter Osapiri Baraza: Waranti wa kukamatwa kwa mwandishi huyo wa habari umetolewa mwezi wa Oktoba mwaka 2013.Baraza anatuhumiwa kushirikiana na maafisa wa serikali kuwayumbisha mashahidi katika kesi dhidi ya Kenyatta na Ruto.Waranti wa kukamatwa kwa Baraza ni wa kwanza kutolewa kuhusu suala la kuyumbisha mashahidi.

Libya

Saif al-Islam Gaddafi mtoto wa marehemu Kanali Muammar Gaddafi wa Libya.

Saif al-Islam Gaddafi mtoto wa marehemu Kanali Muammar Gaddafi wa Libya.

Saif Al - Isalm na Abdullah Al- Senussi - Mtoto huyo wa kiume wa aliekuwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi anashtakiwa katika mahakama ya nchini mwake Libya na haitaki kumfikisha kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC huko The Hague.Anashtakiwa pamoja na mkuu wa usalama wa zamani al-Sanusi kwa kutowa ushirikiano wao katika mauaji na ukandamizaji wakati wa mapinduzi nchini Libya.

Mali

Fatou Bensouda Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahkama ya ICC.

Fatou Bensouda Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahkama ya ICC.

Hapo mwezi wa Januari mwaka 2013 Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Fatou Bensouda ametangaza uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Mali ambao umefanyika kati ya waasi wa itikadi kali za Kiislamu na jeshi la serikali ya Mali kaskazini mwa nchi hiyo. Hadi sasa hakuna kundi linalowajibishwa mbele ya mahakama hiyo ya ICC.

Sudan

Rais Omar Hassan al- Bashir wa Sudan.

Rais Omar Hassan al- Bashir wa Sudan.

Omar Hassan al Bashir anamfuatia Kenyatta kuwa kiongozi wa pili madarakani kushtakiwa na mahakama ya ICC.Hata hivyo tafauti na washtakiwa wa Kenya anagoma kutowa ushirikiano wake kwa mahakama hiyo ya The Hague.

Nchi nyengine pia zinaapuuza waranti wa kumkamata na zinamruhusu Bashir kuingia nchini humo bila ya bughudha.

Kesi dhidi ya waziri Ahmad Muhammad Harun na Abel Raheem Muhammad Hussein na ile nyengine dhidi ya anayedaiwa kuwa mkuu wa kundi la wanamgambo wa Janjaweed Ali Kushayb haikuweza kusikilizwa kwa sababu ya kushindwa kufikishwa washtakiwa mahakamani.

Vingozi wengine wawili wa waasi kutoka Dafur wanaoshtakiwa Abdallah Banda na Saleh Jerbo tayari wamekufa.

Uganda

Kiongozi wa kundi la LRA Joseph Kony.

Kiongozi wa kundi la LRA Joseph Kony.

Joseph Kony,Vincent Otti, Okot Odhiambo na Dominic Ongwen : Waranti wa kukamatwa kwa kiongozi wa kundi la waasi la LRA na makamanda wake wengine watatu tayari ulikuwa umetolewa na mahakama ya ICC tokea mwaka 2005.Hivi karibuni serikali ya Marekani ilitangaza kwamba inausaidia Umoja wa Afrika kwa wanajeshi 120 katika msako wa waasi hao.Kundi la LRA pia limekuwa likiendesha harakati zake kwa muda mrefu mashariki ya Congo,Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Jamhuri ya Afrika ya Kati

Jean-Pierre Bemba aliyekuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Jean-Pierre Bemba aliyekuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Jean- Piere Bemba : Kesi ya Makamo wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilianza hapo mwaka 2010.Bemba anatakiwa ajibu mashtaka ya matumizi ya nguvu yaliofanywa na jeshi lake la waasi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hapo mwaka 2002 na mwaka 2003.Akiwa kama mkuu wa kundi la Vuguvugu la Ukombozi wa Congo (MLC) Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alimuomba asaidie kuzima mapinduzi ya kijeshi nchini humo.Mwishoni mwa mwaka 2013 aliongezewa mashtaka ambapo yeye na wakili wake Aime Kilolo pamoja na wasaidizi wake wengine watatu inasemekana wametowa ushahidi wa uongo na kushawishi mashahidi.

Mwandishi: Maja Braun/ Mohamed Dahman

Mhariri: Mohammed Khelef