1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyombo vya habari Marekani vyamjibu Trump

Isaac Gamba
16 Agosti 2018

 Zaidi ya magazeti 350 nchini Marekani  yamechapisha  Tahariri hii leo  Alhamisi kujibu kauli za rais Donald Trump dhidi ya vyombo vya habari ambavyo amekuwa akivishambulia kwa madai kuwa vinaandika habari za uwongo.

https://p.dw.com/p/33FoZ
USA Tageszeitung The Boston Globe
Picha: Getty Images/AFP/P. Prezioso

Kampeni hiyo ilioongozwa na gazeti moja la kila siku la  mjini Boston inalenga pia kusisitiza juu ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari .

Gazeti hilo la The Boston Globe katika maoni yake ya mhariri limeandika kuwa nchini Marekani hivi sasa wana rais anaye amaini kuwa vyombo vya habari visivyounga mkono sera za serikali yake basi ni maadui wa watu na kuongeza kuwa huu ni mojawapo ya uwongo unaotolewa na rais Trump.  Aidha gazeti hilo limesisitiza kuwa waandishi wa habari sio maadui.

 Gazeti hilo la mjini Boston  limeendelea kuandika kuwa kauli za rais Donald Trump dhidi ya vyombo vya habari pia zinawahamasisha marais wenye misimamo mikali kama vile  Vladimir Putin wa Urusi na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kuwachukulia waandishi wa habari kama maadui.

Kampeni hii ya pamoja ya vyombo vya habari inakuja mnamo wakati rais Trump akiendelea kudai kuwa vyombo vikubwa vya habari vinavyochapisha na kutangaza habari zinazo mkosoa basi vinaandika habari ambazo yeye huziita habari za uwongo.

Wanaharakati wanaotetea uhuru wa vyombo vya habari wanadai kwamba hatua hii ya rais Trump inatishia uhuru wa vyombo vya habari katika kuandika ukweli pamoja na kuikosoa serikali pale vyombo hivyo vinapo kuwa na hisia za matumizi mabaya ya madaraka  serikalini.

 Aidha wanaharakati hao wanadai kuwa hatua hiyo ya Trump inakwenda kinyume na katiba ya  Marekani inayosisitiza juu ya uhuru wa vyombo vya habari.

 

New York Times laandika kurasa saba 

USA Präsident Donald Trump in der Militärbasis Fort Drum
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/C. Kaster

Gazeti la New York Times mojawapo ya magazeti yanayoshambuliwa mara kwa mara na Trump limeandika kurasa saba katika tahariri yake  yenye kichwa cha habari kisemacho " A FREE PRESS NEEDS YOU": au Vyombo huru vya habari vinakuhitaji.

Aidha gazeti hilo limemueleza rais Trump kuwa ukweli asiopenda yeye  kwake ndio anaita "habari za uwongo"  hatua ambayo gazeti hilo limesema ni hatari kwa  demokrasia nchini humo huku pia likisisitiza kuwa kuwaita waandishi wa habari kuwa ni maadui wa watu nayo ni hatari pia.

 Kampeni hiyo ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini Marekani imeungwa pia na vyombo vya habari vingine nchini kote huku pia wanaharakati wa kutetea uhuru wa vyombo vya habari wakisema rais Trump ni kitisho dhidi ya  ya vyombo vya habari.

Ken Paulson mhariri  mkuu wa zamani wa gazeti la "USA Today" yeye kwa upande wake alisema hadhani iwapo vyombo vya habari vitaendelea kukaa kimya  kwani vinapaswa kuchukua hatua pale vinaposhuhudia kiongozi mwenye nguvu kubwa  duniani akijaribu kwenda kinyume na katiba.

Hata hivyo Paulson amehoji iwapo maoni hayo ya wahariri yatafanikiwa lengo lake  na kufikisha ujumbe unaokusudiwa  kwani wanaosoma maoni ya wahariri sio wale wanaowashambulia wakati wa mikutano ya rais.

Paulson amesema vyombo vya habari vinahitaji kampeni kubwa zaidi ya kuelezea kwa upana juu ya umuhimu wa  uhuru wa vyombo vya habari katika jamii ikiwa ni pamoja na kufanyakazi ya ziada ya kufuta imani waliyo nayo baadhi ya wafuasi wa rais  Trump wanaosema kuwa vyombo vya habari havitamuweza Trump.

Hayo yanajiri huku baadhi  wakisema kauli kadhaa za Trump  dhidi ya vyombo vya habari  zimechochea chuki dhidi ya waandishi wa habari wanaohudhuria mikutano yake na pia zinaweza kuwa zimechangia vurugu kama zile zilizofanyika mwezi Juni dhidi ya gazeti  moja la kila siku la Capital   mjini Annapolis katika jimbo la  Maryland Marekani.

Mwandishi : Isaac Gamba/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga