1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Vyama vipi vitaunda serikali ya mseto Pakistan?

Sylvia Mwehozi
12 Februari 2024

Vyama viwili vikubwa vya kisiasa nchini Pakistan viko katika mtanziko juu ya nani atachukua wadhifa wa uwaziri mkuu, baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita kutotoa mshindi wa moja kwa moja na hivyo kulazimika kuungana.

https://p.dw.com/p/4cJxB
Bildkombo | Nawaz Sharif und Imran Khan
Mawaziri wakuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif na Imran KhanPicha: Daniel Leal/Arif Ali/AFP/Getty Images

Mkwamo huo, huenda ukaongeza wasiwasi kuhusu uthabiti wa taifa hilo lenye silaha za nyukilia, ambalo linakabiliwa na mzozo wa kiuchumi na kukabiliana na ongezeko la ghasia za wanamgambo. 

Katika taarifa yake waliyoitoa Jumapili jioni, Chama cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharifcha Pakistan Muslim League-Nawaz, pamoja na kile cha Pakistan Peoples Party PPP cha Bilawal Bhutto Zardari, vilisema kuwa vinajitolea katika "kutanguliza maslahi ya nchi" kuliko kitu chochote na kuliepusha taifa hilo na machafuko ya kisiasa na kuelekea njia ya ustawi na uthabiti.

Pakistan | Uchaguzi wa 2024
Kura zikihesabiwa PakistanPicha: Navesh Chitrakar/REUTERS

Wagombea binafsi ambao wanaungwa mkono na waziri mkuu wa zamani Imran Khanaliyefungwa jela, walipata viti vingi katika uchaguzi wa bunge uliofanyika wiki iliyopita, na hivyo kufifisha nafasi ya chama cha Pakistan Muslim league-Nawaz kuibuka na wingi  wa viti bungeni.

Chama cha Khan cha Tehreek-e-Insaf PTI, kilikaidi ukandamizaji wa miezi kadhaa ambao ulidhoofisha kampeni na kuwalazimu wagombea kuwania kama wagombea binafsi na kisha kuibuka washindi.

Licha ya wagombea binafsi kushinda jumla ya viti 101 katika bunge la kitaifa, serikali nchini humo inaweza kuundwa tu kupitia vyama vinavyotambulika au muungano wa vyama. Hiyo inamaanisha kwamba wagombea hao watapaswa kujiunga na kundi jingine la vyama vidogo ili waweze kuwa kambi yenye ufanisi.

Soma: Pakistan yapongezwa kwa zoezi zuri la uchaguzi

Pakistan
Wafuasi wa chama cha Imran Khan cha Tehreek-e-Insaf (PTI wakiandamana PeshwarPicha: Abdul Majeed/AFP

Ama kwa upande mwingine ni kwamba muungano wa vyama vya PML-N na PPP ambao uliunda serikali ya mseto iliyopita iliyomwondoa mamlakani Khan, huenda vikaibuka kidedea. Vyama vingine sita vidogo vilishinda kiti kimoja au viwili bungeni na huenda vikakaribisha nyongeza ya wagombea binafsi.

Hiyo itatoa fursa ya kupata viti 70 vya ziada vilivyotengwa kwa ajili ya wanawake na dini ndogo na kugawanywa kulingana na matokeo ya uchaguzi. Mwelekeo huo haujawahi kufanyika hapo awali na unakabiliwa na changamoto za kisheria.

Fuatilia ripoti ifuatayo: Matokeo ya awali yawapa ushindi wafuasi wa Imran Khan

Viongozi wa chama cha PTI, wanasisitiza kwamba wamepewa "mamlaka ya watu" kuunda serikali ijayo. Suala la kuhama vyama ni jambo la kawaida nchini Pakistan, angalau wagombea wawili ambao walionyesha utiifu kwa Khan kabla ya uchaguzi, tayari wametangaza kujiunga na chama cha PML-N.

Wanachama wengi zaidi wa zamani wa PTI ambao hawakushinda viti pia wanapinga matokeo hayo mahakamani, jambo ambalo linaweza kuzorotesha zaidi mazungumzo ya muungano.