Vita Iran vyakwamisha dawa kutoka India kwenda Afrika
2 Juni 2026
India, ambayo mara nyingi huitwa "duka la dawa la nchi zinazoendelea," ndiyo msambazaji mkuu wa dawa zinazoagizwa kutoka nje barani Afrika. Takwimu zinaonyesha kuwa takribani asilimia 40 ya dawa zote zinazoingizwa Afrika hutoka India. Dawa hizo husafirishwa kupitia vituo vikubwa vya usafirishaji vya Dubai, Doha na Abu Dhabi kabla ya kufika katika bandari na viwanja vya ndege vya Afrika.
Lakini tangu vita kati ya Iran na Marekani kuathiri usafiri katika eneo la Hormuz, gharama za usafirishaji zimeongezeka, baadhi ya safari za ndege zimepunguzwa na meli nyingi zinalazimika kubadili njia.
Hali hiyo imeanza kuathiri minyororo ya ugavi wa dawa duniani. Daktari Rajeev Jayadevan, mtaalamu wa afya na mawasiliano ya afya kutoka India, anasema minyororo ya ugavi wa dawa inayounganisha Asia na Afrika ni ya kimataifa na inategemea usafirishaji wa uhakika.
"Kidonge kinachotumiwa na mgonjwa barani Afrika kinaweza kabisa kuwa kimetengenezwa nchini India kwa kutumia viambato hai vya dawa (APIs) vilivyoagizwa kutoka China, kisha kusafirishwa kupitia njia za kimataifa za biashara ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu."
Wagonjwa huenda wakakabiliwa na ucheleweshaji wa dawa
Kwa maneno mengine, kidonge kinachotumiwa na mgonjwa nchini Kenya, Tanzania au Nigeria kinaweza kuwa kimetengenezwa India kwa kutumia malighafi kutoka China na kusafirishwa kupitia njia za biashara zinazopita Ghuba ya Uajemi. Kuvurugika kwa njia hizi kunamaanisha kuwa wagonjwa wanaweza kuanza kukabiliwa na ucheleweshaji wa dawa au hata uhaba wa baadhi ya bidhaa muhimu.
Wataalamu wanasema hatari ni kubwa zaidi kwa dawa zinazohitaji kuhifadhiwa katika hali maalumu za joto, kama chanjo, insulini na baadhi ya dawa za kibaolojia. Afrika, tofauti na Ulaya au Marekani, haina akiba kubwa ya dawa za matumizi ya miezi kadhaa, jambo linaloifanya kuwa katika hatari zaidi wakati minyororo ya usambazaji inapovurugika.
Kwa upande wake, Javin Bhinde, mtaalamu wa sekta ya dawa na mkurugenzi wa kampuni ya ushauri ya SynCore nchini India, anasema ushirikiano wa muda mrefu kati ya India na Afrika umewezesha mamilioni ya watu kupata dawa za gharama nafuu.
"Kwa upande wa dawa za matibabu, India na Afrika zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu, wenye manufaa kwa pande zote mbili, ambapo India imekuwa ikiisambazia Afrika kiasi kikubwa cha dawa za gharama nafuu."
Bhinde anasema kampuni nyingi za dawa za India zimewekeza barani Afrika ili kuimarisha upatikanaji wa dawa, lakini mgogoro wa sasa umeonyesha jinsi mfumo huo unavyobaki kuwa dhaifu mbele ya misukosuko ya kimataifa.
Hofu ya uhaba wa dawa inakuja wakati ambapo Shirika la Afya Duniani limesema zaidi ya nusu ya nchi za Afrika tayari zinakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya. Kwa madaktari na wagonjwa, kuchelewa kwa dawa za kifua kikuu, UKIMWI, kisukari au shinikizo la damu kunaweza kuwa na madhara makubwa, na wakati mwingine kuhatarisha maisha.