1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Mubashara
MigogoroKimataifa

Vita Iran: Israel yamuua mkuu wa usalama Iran Ali Larijan

Iddi Ssessanga AP, AFP, REUTERS, DPA
Imechapishwa 17 Machi 2026ilisahihishwa mwisho 17 Machi 2026

Israel imesema imewaua mkuu wa juu wa usalama wa Iran Ali Larijani na kiongozi wa kikosi cha Basij Gholamreza Soleimani katika mashambulizi ya anga, lakini Iran bado haijathibitisha vifo vyao.

https://p.dw.com/p/5AX9K
Lebanon, Beirut 2025 | Katibu wa Baraza la Usalama la Iran Ali Larijani katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na Spika wa Bunge Berri.
Inaripotiwa kuwa Larijani alikuwa kinara wa ukandamizaji mkali wa maandamano nchini Iran mapema mwaka huuPicha: Marwan Naamani/ZUMAPRESS/picture alliance
Ruka sehemu inayofuata Unachohitaji kujua

Unachohitaji kujua

  • Iran bado haijathibitisha vifo vya maafisa hao wawili
  • Jeshi la Israel limesema afisa mkuu wa usalama wa Iran Ali Larijani na kiongozi wa Basij Gholamreza Soleimani wameuawa katika mashambulizi
  • Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad washambuliwa katika shambulizi la makombora na droni
  • Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu zazima droni na makombora zaidi kutoka Iran
  • Vipande vya makombora vilivyoanguka vimesababisha kifo cha mtu mmoja mjini Abu Dhabi
  • Israel yaanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya malengo mjini Tehran na mji mkuu wa Lebanon, Beirut
  • Rais wa Marekani Donald Trump amezitaka nchi kujihusisha haraka na kwa hamasa kubwa kulinda usafirishaji katika Mlango-Bahari wa Hormuz
  • Ujerumani, Hispania na Italia zimekataa kutoa msaada wa kijeshi kusindikiza meli kupita katika njia hiyo ya maji
  • Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran “si vita vya Ulaya”

Huu hapa ni muhtasari wa matukio makuu katika vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Machi 17:

Ruka sehemu inayofuata Netanyahu asema kuuawa kwa Larijani kunaweza kufungua njia kwa Wairan kuiasi serikali
17 Machi 2026

Netanyahu asema kuuawa kwa Larijani kunaweza kufungua njia kwa Wairan kuiasi serikali

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuuawa kwa afisa mkuu wa usalama wa Iran Ali Larijani kunaweza kuwa hatua nyingine itakayowawezesha Wairani kuasi dhidi ya serikali yao.

“Leo asubuhi tulimuondoa Ali Larijani, mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi, kundi la wahalifu ambalo kwa hakika linaiendesha Iran,” alisema Netanyahu.

Netanyahu aliongeza kuwa uasi dhidi ya serikali “hautafanyika mara moja wala hautakuwa rahisi. Lakini tukidumu katika hili — tutawapa nafasi ya kuchukua hatima yao mikononi mwao.”

Iran bado haijathibitisha kifo cha Larijani.

https://p.dw.com/p/5AYR6
Ruka sehemu inayofuata Tunajua nini kuhusu Ali Larijani?
17 Machi 2026

Tunajua nini kuhusu Ali Larijani?

Lebanon Beirut | Ali Larijani
Ali Larijani akihudhuria tukio kwenye kaburi la kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah mjini Beirut, Lebanon, Septemba 27, 2025.Picha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Madai ya Israel kwamba imemuua Ali Larijani bado hayajathibitishwa na vyanzo vya nje wala kukubaliwa na utawala wa Tehran, lakini ni nani katibu huyo mwenye umri wa miaka 67 wa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa?

Larijani ni sehemu ya familia ya wanazuoni wakuu wa dini ambayo jarida la Time liliwahi kuieleza kama “Kennedy wa Iran.”

Hata hivyo, tofauti na jamaa zake wengi wa karibu, hakuchagua njia ya kupata madaraka kupitia ngazi za kidini kama ayatollah.

Badala yake, Larijani alijiunga kwanza na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran kabla ya kusoma falsafa na baadaye kuingia kwenye siasa, akianza kama waziri wa utamaduni na kisha kupanda katika nyadhifa mbalimbali.

Kwa hiyo, hakuwahi kustahili kumrithi Ayatollah Khamenei kutokana na kukosa sifa za kidini, lakini alionekana kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa usio rasmi baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel mwishoni mwa Februari yaliyoua sehemu kubwa ya uongozi wa juu wa Iran.

Kwa maelezo zaidi, soma uchambuzi wa kina wa mwandishi wa DW Darko Janjevic ulioandikwa mapema mwezi huu.

https://p.dw.com/p/5AYNP
Ruka sehemu inayofuata Mashambulizi dhidi ya bandari UAE yaathiri shughuli za uendeshaji
17 Machi 2026

Mashambulizi dhidi ya bandari UAE yaathiri shughuli za uendeshaji

Umoja wa Falme za Kiarabu, Fujairah 2026 | Familia mbele ya karakana ya meli katika Mlango wa Hormuz
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya mataifa ya Ghuba yamesababisha mauzo ya mafuta kutoka kanda hiyo kushuka kwa kiasi kikubwa.Picha: Giuseppe Cacace/AFP

Upakiaji wa mafuta katika bandari ya Fujairah ya Umoja wa Falme za Kiarabu ulitatizika Jumanne kufuatia shambulizi na moto uliozuka katika kituo cha usafirishaji wa nje, huku Iran ikiendelea na mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya nchi za Ghuba.

Mamlaka za eneo hilo zilisema hakuna majeruhi walioripotiwa katika shambulizi hilo, ambalo ni la tatu ndani ya siku nne.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa upakiaji wa mafuta ghafi ulisimamishwa katika kituo hicho, vikinukuu vyanzo vilivyo karibu na tukio.

Shughuli katika uwanja wa gesi wa Shah — ulioko kilomita 180 kusini-magharibi mwa Abu Dhabi — ziliendelea kusitishwa kufuatia shambulizi la awali la droni.

Bandari nyingine za usafirishaji wa nje za UAE ziko ndani ya Ghuba, ambayo kwa sasa imekatishwa kwa kiasi kikubwa na masoko ya kimataifa kutokana na udhibiti wa Iran wa Mlango-Bahari wa Hormuz, ambako kwa kawaida hupitia karibu humusi moja ya mafuta ya dunia.

Nchi za Ghuba zimeathirika zaidi na hatua za kulipiza kisasi za Iran kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yaliyochochea vita vya sasa, huku Tehran ikilenga mali za Marekani katika kanda hiyo pamoja na miundombinu ya kiraia.

https://p.dw.com/p/5AXuU
Ruka sehemu inayofuata Iraq iko kwenye mazungumzo na Iran kuruhusu meli zake za mafuta kupita katika Mlango wa Hormuz
17 Machi 2026

Iraq iko kwenye mazungumzo na Iran kuruhusu meli zake za mafuta kupita katika Mlango wa Hormuz

Oman, Shinas 2026 | Tanker la gesi ya LPG likiwa limetia nanga katika Mlango wa Hormuz
Usafirishaji wa meli katika Mlango wa Hormuz umekaribia kusimama kutokana na vita na tishio la mashambulizi ya IranPicha: Benoit Tessier/REUTERS

Waziri wa Mafuta wa Iraq, Hayyan Abdul-Ghani, amesema serikali ya Iraq iko katika mawasiliano na Iran ili kuruhusu baadhi ya meli zake za mafuta kupita katika Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Iraq (INA).

Usafirishaji wa meli duniani umekaribia kusimama katika njia hiyo muhimu kutokana na vita na tishio la mashambulizi ya Iran.

Takribani humusi moja ya usafirishaji wa mafuta duniani hupita katika mlango huo ulioko karibu na pwani ya Iran.

Wakati huo huo, bei ya mafuta ilipanda kwa zaidi ya asilimia 5 kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa meli za mizigo kupita katika Mlango wa Hormuz.

Takribani saa 06:15 GMT, kipimo cha mafuta cha Marekani cha West Texas Intermediate kilipanda kwa asilimia 5.16 hadi dola 98.32 kwa pipa, huku mafuta ya Brent pia yakipanda zaidi ya asilimia 5 kabla ya kushuka tena.

Marekani imezitaka nchi washirika kusaidia kulinda Mlango wa Hormuz.

https://p.dw.com/p/5AXtj
Ruka sehemu inayofuata China yazingatia ufafanuzi wa Trump kuhusu kuahirisha ziara Beijing
17 Machi 2026

China yazingatia ufafanuzi wa Trump kuhusu kuahirisha ziara Beijing

China imesema imezingatia ufafanuzi wa Marekani kuhusu mipango ya Rais Donald Trump kuahirisha ziara yake iliyopangwa Beijing kwa mkutano na Rais Xi Jinping. Ziara hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika kati ya Machi 31 na Aprili 2.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, amesema Marekani imekanusha taarifa za vyombo vya habari zilizodai kuwa ziara hiyo inahusishwa na suala la usalama wa usafiri katika Mlango wa Hormuz, huku akisisitiza kuwa mawasiliano kati ya nchi hizo mbili yanaendelea.

Wakati huo huo, maafisa wa juu wa biashara wa Marekani wamekuwa wakikutana na wenzao wa China mjini Paris kujadili masuala ya biashara na maandalizi ya mkutano wa viongozi hao.

Ujerumani, China zauteteta mkataba wa Iran

Trump amesema aliomba ziara hiyo iahirishwe kwa muda wa takriban mwezi mmoja ili aweze kubaki Washington wakati vita dhidi ya Iran vinaendelea.

Hapo awali alidokeza kuwa hali ya ziara hiyo ingeweza kutegemea iwapo China ingesaidia kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz, lakini Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent baadaye alikanusha uhusiano huo na kuutaja kama simulizi lisilo sahihi.

https://p.dw.com/p/5AXre
Ruka sehemu inayofuata Israel imesema kiongozi wa Basij, Gholamreza Soleimani, ameuawa katika shambulizi
17 Machi 2026

Israel imesema kiongozi wa Basij, Gholamreza Soleimani, ameuawa katika shambulizi

Israel imesema imemuua kiongozi wa kikosi cha kujitolea cha Basij kinachohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Gholamreza Soleimani, katika shambulizi lililofanywa Jumatatu, hatua inayochukuliwa kama pigo kubwa kwa vikosi vinavyotumika kudhibiti maandamano nchini Iran.

“Jana (Jumatatu), Jeshi la Anga la Israel, likitekeleza operesheni kwa kuzingatia taarifa za kijasusi za Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), lilimlenga na kumuua Gholamreza Soleimani, ambaye alikuwa akifanya kazi kama kamanda wa kikosi cha Basij kwa miaka sita iliyopita,” jeshi la Israel lilisema.

Kwa mujibu wa jeshi la Israel, Basij imekuwa sehemu muhimu ya mfumo wa usalama wa Iran na chini ya uongozi wa Soleimani imeongoza operesheni za ukandamizaji dhidi ya waandamanaji, zikiwemo matumizi ya nguvu kupita kiasi na kukamatwa kwa watu wengi.

Hata hivyo, hadi sasa Iran haijathibitisha taarifa za kifo cha kiongozi huyo, wakati mvutano wa kijeshi ukiendelea kuongezeka katika kanda ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/5AXpq
Ruka sehemu inayofuata Israel yadai kumuua mkuu wa usalama wa Iran Ali Larijani
17 Machi 2026

Israel yadai kumuua mkuu wa usalama wa Iran Ali Larijani

Iran, Tehran 2026 | Maandamano ya Siku ya Al-Quds yakimshirikisha Ali Larijani mjini Tehran
Ali Larijani akishiriki katika maandamano ya jadi ya Siku ya Quds katika mji mkuu Tehran, Ijumaa Machi 13, 2026. Picha: Iranian President's Press Office/UPI Photo/IMAGO

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema afisa mkuu wa usalama wa Iran Ali Larijani ameuawa katika shambulizi lililofanyika usiku.

Iran bado haijathibitisha kifo cha Larijani.

Larijani ni katibu wa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa nchini Iran, linalosimamia uratibu wa masuala ya ulinzi na sera za kigeni.

Inaaminika kuwa Larijani ndiye mhusika mkuu wa ukandamizaji mkali wa waandamanaji uliofanywa na serikali ya Iran mapema mwaka huu.

Hata hivyo, akaunti za Larijani kwenye X na Telegram zilichapisha ujumbe ulioandikwa kwa mkono kuhusu mabaharia wa Iran waliouawa katika shambulizi la torpedo la Marekani baharini.

Ujumbe huo unasema kumbukumbu ya mabaharia hao “itabaki milele katika moyo wa taifa la Iran.”

Chapisho hilo halithibitishi kifo cha Larijani kama ilivyodaiwa na Israel, na haijulikani ni lini ujumbe huo, unaodhaniwa kuwa kwa maandishi yake, uliandaliwa.

https://p.dw.com/p/5AXky
Ruka sehemu inayofuata Roketi, droni, vyalenga ubalozi wa Marekani Baghdad
17 Machi 2026

Roketi, droni, vyalenga ubalozi wa Marekani Baghdad

Iraq, Baghdad 2026 | Moshi juu ya Ubalozi wa Marekani baada ya shambulizi la droni katika Ukanda wa Kijani
Wanamgambo wenye makao yao Iraq na wanaohusishwa na Iran wamekuwa wakilenga maeneo ya Marekani nchini humo tangu vita vilipoanzaPicha: AFP/Getty Images

Makombora na droni vililenga Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad mapema Jumanne, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama vya Iraq.

Maafisa walisema mifumo ya ulinzi wa anga wa Iraq ulidungua droni na makombora kadhaa bila kuripotiwa majeruhi, lakini vipande vya makombora viligonga eneo la ubalozi, kusababisha mlipuko na moshi mkubwa kuonekana angani.

Wakati huo huo, shambulizi jingine lilipiga nyumba ndani ya eneo lenye ulinzi mkali la Ikulu katika eneo la al-Jadriya mjini Baghdad.

Wanamgambo wanaohusishwa na Iran wanaoishi Iraq wanashukiwa kuhusika na mashambulizi hayo, ambayo yamekuwa yakilenga mara kwa mara maslahi ya Marekani nchini humo.

https://p.dw.com/p/5AXCW
Onesha matokeo zaidi