1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kiafrika wakutana na Macron

18 Mei 2021

Mkutano wa kilele baina ya Afrika na Ufaransa unatarajiwa kutoa fursa kwa Afrika kupata msaada wa kifedha kukabiliana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la Covid-19

https://p.dw.com/p/3tXvo
Frankreich Emmanuel Macron und Abdalla Hamdok
Picha: Ludovic Marin/AFP

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewakaribisha viongozi wa nchi za Afrika na wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa katika mkutano wa kilele utakaotoa nafasi ya kulipatia bara hilo msaada wa kifedha kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19.

Mkutano unaongozwa na rais Emmanuel Macron umeshaanza na unaendelea na wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa wanaohudhuria ni mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF Georgieva Kristalina pamoja na mkurugenzi mkuu wa benki ya dunia Axel Van Trotsenburg.

Mkutano huo utamalizika leo jioni kwa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na rais Macron pamoja na rais wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kondo Felix Tshisekedi ambaye nchi yake inashikilia nafasi ya kupokezana ya mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Hadi sasa nchi za Afrika hazijaathirika sana na janga la virusi vya Corona kama hali ilivyo katika nchi nyingine za dunia.

Frankreich Paris | Treffen | Macron und al-Sisi
Picha: Eliot Blondet/ABACA/picture alliance

Mpaka sasa waliokufa kutokana na Covid-19 barani Afrika ni jumla ya watu 130,000 lakini gharama za kiuchumi ziko wazi kabisa ambapo shirika la fedha la kimataifa lilionya mnamo mwishoni mwa mwaka 2020 kwamba bara hilo la Afrika linakabiliwa na upungufu wa fedha wa dolla bilioni 290 zinazohitajika kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya baadae kufikia mwaka 2023.

Mwaka jana mnamo mwezi Aprili nchi tajiri za kundi la G20 na klabu ya Paris ambalo ni kundi la nchi wakopeshaji zinazojaribu kutafuta suluhisho endelevu kwa nchi zenye madeni,zilikubaliana kusitisha kwa muda tozo ya riba kwa madeni ya umma na hatua hiyo ilipokelewa vizuri ingawa ni hatua ambayo haitoshi. Nchi nyingi zinataka hatua hiyo ya kutotozwa riba ya madeni kuyahusisha madeni yote ya nje hadi litakapomalizika janga hili.

Mwezi uliopita rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kwamba nchi tajiri kwa pamoja ziko kwenye mchakato wa kulitupa mkono bara la Afrika kwa kupitia suluhisho la njia ambazo zimepitwa na wakati za tangu miaka ya 1960 na kutahadharisha kwamba hatua ya kushindwa kuzisaidia nchi hizo zitachangia kupunguza fursa za kiuchumi,na kuzusha wimbi la ghafla la wahamiaji na hata kutanua ugaidi.

Frankreich Präsident Emmanuel Macron & Paul Kagame, Präsident Ruanda
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Rais wa benki ya maendeleo ya nchi za Magharibi mwa Afrika BOAD-  Serge Ekue,ameliambia shirika la habari la AFP kwamba bara la Afrika linahitaji mikopo ya muda mrefu zaidi inayopindukia miaka 7 na viwango yenye viwango vya riba vya asilimia 3 kuliko ile inayotozwa viwango vya riba ya zaidi ya asilimi 6.

Mkutano huo wa kilele unaoendelea umekuja siku moja baada ya kikao kilichohudhuriwa na viongozi wengi wa nchi ambacho kililenga kuiunga mkono serikali ya Sudan inayoongozwa na waziri mkuu Abdallah Hamdok iliyoko kwenye kipindi chake cha mpito baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa muda mrefu  Omar al-Bashir.

Rais Macron alitangaza katika mkutano wa jana Jumatatu kwamba nchi yake itaifutia madeni ya kiasi dolla bilioni 5 Sudan ili kuisaidia serikali hiyo ya mpito.

Na mkutano wa leo unaohudhuriwa na viongozi wengi wa nchi za Afrika ndio mkubwa zaidi wa ana kwa ana wa viongozi wa ngazi za juu unaofanyika katika kipindi hiki cha janga la Covid-19.Rais Paul Kagame wa Rwanda nae ni miongoni mwa marais wanaohudhuria pamoja na rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW