Viongozi wa ECOWAS kukutana na Jammeh | Matukio ya Afrika | DW | 13.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Viongozi wa ECOWAS kukutana na Jammeh

Ujumbe wa wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, uko ziarani nchini Gambia, kwa lengo la kumshawishi Rais Yahya Jammeh akubali kuwa alishindwa katika uchaguzi wa Disemba Mosi.

Ziara hiyo inafanyika siku kadhaa, baada ya Rais Jammeh kutangaza nia yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mpinzani wake Adama Barrow. Ujumbe huo unawajumuisha Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS, Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, Rais Alpha Conde wa Guinea pamoja na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari.

Umoja wa Afrika unapinga vikali kitendo cha Jammeh kubatilisha msimamo wake wa awali ambapo alisema kuwa kayakubali matokeo hayo. Taarifa ya viongozi hao imemtaka Jammeh kuheshimu maamuzi ya wananchi wa Gambia. Ujumbe huo leo unatarajiwa kufanya mazungumzo na rais mteule wa Gambia, Adama Barro pamoja na wajumbe wa muungano wa upinzani, ambao walimuunga mkono Barrow katika urais.

Hapo jana muungano huo ulimtaka Jammeh aondoke mara moja madarakani na kukabidhi madaraka kwa Barrow. Mjumbe wa kamati kuu katika muungano wa upinzani, Ahmed Fatty, amewaambia waandishi wa habari mjini Banjul kwamba Jammeh hakuyapinga matokeo hayo kisheria. Jammeh alisema atafungua shauri mahakamani kuyapinga matokeo hayo.

Gambia Banjul Anhänger Adama Barrow (Reuters/T. Gouegnon)

Wananchi wa Gambia washeherekea matokeo ya uchaguzi mjini Banjul

Fatty amesema Gambia kwa sasa haina Mahakama ya Juu kuweza kusikiliza pingamizi hilo na kwamba Jammeh akiwa kama kiongozi anayendoka madarakani, hawezi kumteua jaji wa Mahakama ya Juu, wakati wa siku zake za mwisho ofisini.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limemtaka Jammeh kukutana na wapatanishi wa kimataifa ambao wako ziarani Gambia kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, Mohamed Ibn Chambas anatarajiwa kuwasili leo mjini Banjul.

Naibu Balozi wa Uhispania, Juan Manuel Gonzalez de Linares, amesema wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wanamtaka Rais Jammeh kukubali kukutana na kushirikiana na ujumbe huo wa ECOWAS na Umoja wa Mataifa. Uhispania ndiyo mwenyekiti wa baraza hilo kwa mwezi huu.

Baraza hilo limekutana kutokana na ombi la Senegal la kutaka kuujadili mzozo wa Gambia, baada ya Jammeh kukataa kuyatambua matokeo hayo. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power amesema hali inayoendelea Gambia inatishia usalama wa nchi hiyo, akizinukuu taarifa kwamba baadhi ya maafisa wa kijeshi , wanamuunga mkono Jammeh.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA

Mhariri: Josephat Charo