Viongozi duniani walaani shambulio la Kabul | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi duniani walaani shambulio la Kabul

Viongozi mbalimbali duniani wamelaani  vikali shambulizi la bomu  lilotokea mapema leo mjini Kabul nchini Afghanistan katika eneo la balozi mbalimbali na majengo muhimu ya serikali.

Viongozi mbalimbali duniani wamelaani  vikali shambulizi la bomu  lilotokea mapema leo mjini Kabul nchini Afghanistan katika eneo la balozi mbalimbali na majengo muhimu ya serikali. Idadi ya waliofariki kufutia shmabulizi hilo  imeongezeka na kufikia watu 80 na wengine 350 kujeruhiwa.Bomu hilo lilikuwa limetegwa kwenye gari.Akizungumza katika mji wa Nuremberg hapa Ujerumani  kansela Angela Merkel amesema shambulizi hilo ni ishara kuwa ugaidi hauna mipaka. Polisi imethibitisha kuwa mlipuko huo ulitokea karibu sana na ubalozi wa Ujerumani,na wafanyakazi kadhaa wa ubalozi huo ni miongoni mwa waliojeruhiwa.Merkel amesema vita dhidi ya ugaidi vitaendelea.Sote kwa pamoja, tunaoamini haki,Uhuru na hadhi ya binadamu barani ulaya, Marekani, Afrika pamoja  na  Afghanistan tutaendelea na mapambano dhidi ya magaidi na tutashinda

Afghanistan Explosion in Kabul (Reuters/M. Ismail)

Polisi wa Afghanistan katika eneo la shambulizi

.China ,Ufaransa na Uturuki zimesema hakuna mfanyakazi wake hata mmoja alijeruhiwa kufuatia shambulio hilo ambapo idadi kubwa ya waliofariki ni raia wa Afghanistan.Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu  amesema wameanza kuwaondoa raia wake mji  Kabul baada ya kuharibiwa vibaya ubalozi wake.Waziri huyo  ametaka uchunguzi  kamili ufanyike kuhusu jinsi gari hilo lilokuwa na bomu lilivyoweza kufika mjini Kabul ambako kuna ulinzi mkali kutokana na kuwa na makaazi ya wanadiplomasia."Nimekuwepo kwenye mji huo mara nyingi .Hili ni shambulizi baya.Sielewi vipi  gari hilo liliweza kupita vizuizi mbalimbali vya polisi.Tumshukuru mungu hakuna mfanyakazi yeyote wa ubalozi wetu aliyejeruhiwa. Tutawatuma  wachunguzi wetu nchini Aghanistan kukusanya ripoti kamili kuhusu shambulizi hilo. Lakini kwa mara nyingine tunalaani shmabulizi hilo la kigaidi na tutaendelea  kuwasaidia ndugu zetu Waafghanistan."Ubalozi wa Marekani mjini Kabul  na  ujumbe wa jumuiya ya Nato nchini humo umelaani vikali shambulizi hilo ambalo limetajwa kuwa baya zaidi  tangu kuondoka majeshi ya kigeni nchini humo mwishoni mwaka 2014.

Afghanistan Explosion in Kabul (Getty Images/AFP/S. Marai)

Wingu la moshi mkubwa katika eneo kulikotokea mlipuko huo wa bomu

Hadi sasa haifahamiki kwanini shambulizi hilo lililenga eneo la Wazir Akbar Khan, na hakuna kundi lilojitokeza kudai kuhusika ingawa  wapiganaji wa Taliban na wale wa IS wamekuwa  wakiwahangaisha raia hasa katika mji huo wa Kabul. Vikosi vya Marekani na vile vya Afghanistan  vimekuwa vikakabiliana na uasi wa kundi la Taliban kwa zaidi ya miaka 15. Marekani kwasasa ina zaidi ya majeshi elfu 8 nchini humo,na imekuwa ikitoa mafunzo  kwa wanajeshi wa  Afghanistan na pia kuhusika na operesheni za kukabiliana na magaidi.
Mwandishi:Jane Nyingi
Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com