1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vyapandisha bei ya mafuta

Yusra Buwayhid
23 Aprili 2019

Uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuziwekea vikwazo nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran umeibua wasiwasi kuhusu usambazaji wa kimataifa wa mafuta ghafi, huku bei ya mafuta ikiwa imepanda kwa kiasi kikubwa.

https://p.dw.com/p/3HFcx
Iran Erdölindustrie bei Teheran
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi

Marekani Jumatatu imezitaka nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran zisite kufanya hivyo kuanzia Mei 1, au zitakabiliwa na vikwazo. Uamuzi huo utamaliza muda wa miezi sita ambapo nchi nane nyingi kutoka bara la Asia, ziliruhusiwa kununua mafuta hayo kutoka Iran.

Wataalamu wa sekta hiyo wamesema Jumatatu, kuwa vikwazo hivyo vinaweza kupelekea kupungua kwa hadi mapipa milioni 1.2 ya mafuta katika soko la kimataifa.

Idadi hiyo inaweza ikawa ndogo zaidi kulingana na jinsi nchi zitakavyoupokea uamuzi huo wa Marekani, na kiasi cha mafuta ambacho Iran itaenedelea kusafirisha.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema anataka kusambaratisha mapato ya Iran yanayotokana an mauzo ya mafuta. Trump anaamini fedha hizo zinatumiwa na Iran kufadhili shughuli za uharibifu katika Mashariki ya Kati na kwengineko.

Persischer Golf Ölplattform
Picha: Reuters/R. Homavandi

Uamuzi huo unamaanisha ruhusa ya kununua mafuta kutoka Iran haitoongezwa muda wake utakapomalizika Mei 2 kwa mataifa matano tofauti; China na India pamoja na washirika wa Marekani Japan, Korea Kusini na Uturuki.

Uturuki yakosoa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ameikosoa hatua hiyo ya Marekani ya kuziwekea vikwazo nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran, akisema itahatarisha  utulivu wa eneo zima.

"Kisiasa sio uamuzi sahihi. Kimaadili sio haki. Kwa mtazamo wa kibiashara, pia sio sawa. Na pia ni kinyume na sheria ya kimataifa ya biashara, na ni kinyume na sheria za Shirirka la Biashara Duniani na ni hatari kwa kanda nzima. Nani atakaefaidika? Badala yake bei ya mafuta itaongezeka katika nchi zinazoshirikiana kwa karibu na Marekani. Uamuzi huu haujawahi kushuhudiwa duniani hadi sasa," amesema Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki.

Waziri wa Mafuta ya Petroli na Gesi Asilia wa India Dharmendra Pradhan,  amesema Jumanne kuwa nchini hiyo itatumiwa mafuta ya ziada kutoka nchi nyingine zinazochimba mafuta, ili kufidia pengo litakalojitokeza kwa kukosa mafuta ya Iran.

Saudi Arabia, msafirishaji mkubwa wa mafuta duniani, ilisema jana kwamba itashirikiana na nchi nyingine zinazochimba mafuta kuhakikisha kuna usambazaji wa kutosha wa mafuta ghafi katika soko la kimataifa.