1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana wakutana Rwanda kuzungumzia changamoto na fursa

20 Juni 2022

Vijana kutoka nchi 54 zinazounda jumuiya ya madola wanakutana mjini Kigali siku mbili kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali kutoka nchi za jumuiya ya madola.

https://p.dw.com/p/4CwF9
Ruanda Kigali | vor Commonwealth Gipfeltreffen
Picha: Luke Dray/Getty Images

Mazungumzo kwenye mkutano huu mkubwa yanazingatia hasa nafasi ya vijana katika uongozi wa mataifa yao. Hata hivyo vijana wamelaumiwa kuwa baadhi yao ni kama wanajizuia kuingia moja kwa moja kwenye mifumo ya uongozi na siasa kwa sababu ambazo hazijafahamika hadi sasa.Vijana 10,000 wa Afrika washiriki kongamano lao Kigali Rwanda

Wazungumzaji wanasema mataifa ya jumuiya ya madola na serikali zake kwa kiasi fulani yamejaribu kuweka mikakati kadhaa inayoratibu maendeleo ya vijana katika sekta za elimu,uongozi bora, uchumi na biashara pamoja na siasa kwa ujumla.

Lakini kwa baadhi ya vijana ni kama hilo haliwahusu.Vijana wanakiri madai na wanasema kwamba kukutana kwao katika kundi kubwa kama hili la jumuiya ya madola ni fursa muhimu ya kuleta mapinduzi katika suala zima la kukabiliana na changmoto zinazowakabili.

Ruanda Jugendliche Treffen in Kigali zu dreitägiger Konferenz
Mkutano wa vijana uliofanyika Kigali mwaka 2019Picha: DW/Sylvanus Karemera

Cecelia Martina ni mmoja wa vijana wanaohudhuria mkutano huu anasema kuwa; "Nadhani utamaduni ni jambo linalounganisha watu pamoja,na mazungumzo na midahalo kama huu inatusaidia sisi kama vijana kufahamu utamaduni ulioko miongoni mwetu kwa sababu ukishaelewa utamaduni wa mwenzako mnaheshimiana na hatimaye hilo linawafikisha katika hatua ya kushirikiana na kupiga hatua pamoja."

Mkutano huu unafanyika chini ya kauli mbiu inayowataka vijana kumiliki mstakabali wao wa baadaye, suala ambalo limemfanya waziri wa vijana wa Rwanda Rosemary Mbabazoi kuwapa vijana hawa changamoto

"Je mstakabali wenu umo mikononi mwenu au umo mikononi mwa watu wengine? Je mpo kuchukua jukumu lenu au mnamwachia mtu mwingine awafanyie mambo...je mpo tayari kufanya maamuzi ya vitu mnavyotaka kufanya au mnakalia kusubiri kesho,kesho kutwa,mtondo mtondogoo hadi miezi na miaka?je mpo? au mnaendelea kuahirisha?"

Tayari sekretarieti ya jumuiya ya madola imetangaza kuanzisha mtandao mpya wa vijana chini ya miaka 35 ambao wajumbe wake watashirikiana kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja za afya,biashara na uchumi,siasa,uongozi na uharibifu wa mazingira.