1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Vifo vya tetemeko Uturuki na Syria vyafikia 9,500

Lilian Mtono
8 Februari 2023

Juhudi za kuwaokoa watu waliokwama kwenye vifusi zimeendelea nchini Uturuki na Syria baada ya tetemeko kubwa ambalo hadi hii leo limesababisha vifo vya watu zaidi ya 9,500.

https://p.dw.com/p/4NDrm
Syrien Erdbeben Rettungsarbeiten Aleppo
Picha: BAKR ALKASEM/AFP

Kwa siku mbili mfululizo, tangu tetemeko hilo la kubwa kabisa la ardhi nchini Uturuki na Syria, vikosi vya uokozi vimekuwa vikifanya juhudi ya kuokoa watu katikati ya mazingira magumu ya baridi kali na mitetemo zaidi ili kuwanasua ambao bado wamekwama.

Picha za kusikitisha zimeendelea kusambaa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zinazoonyesha watu wakiokolewa kutoka kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Miongoni mwa picha hizo inaonyesha waokoaji hao wakishangilia baada ya kumuokoa mtoto mchanga akiwa mzima wa afya, lakini kwa upnade mwingine picha ya kusikitisha ya baba mmoja aliyeshika mwili wa bintiye ambaye tayari alikuwa amefariki.

Soma Zaidi: Tetemeko Uturuki na Syria: Waokoaji waendelea na kazi usiku kucha

Taarifa rasmi zinasema hadi sasa watu 6,957 wamefariki dunia kufuatia janga hilo nchini Uturuki na 2,547 huko Syria na kufanya idadi jumla kuwa 9,504, huku kukiwa na wasiwasi wa idadi hiyo kuongezeka mara mbili. Taarifa za Mamlaka ya kupambana na Majanga ya Uturuki imesema leo kwamba zaidi ya watu 38,000 wamejeruhiwa nchini humo.

Syrien | Bashar Assad und Recep Tayyip Erdogan
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Utruki na Bashar al-Assad wa Syria katika picha ya pamoja mnamo mwaka 2010. Sasa wakuu hawa wanakabiliwa na janga kubwa kwenye mataifa yao baada ya tetemeko kubwa.Picha: Bassem Tellawi/AP/picture alliance

Nchini Syria serikali imesema inaendelea kuhamasisha kila mmoja kuunga mkono jitihada za kuwasaidia wahanga wa tetemeko hilo, ambazo hata hivyo imekiri zinaweza kuzuiwa na mzingiro wa magaidi na vizuizi vya magharibi, hii ikiwa ni kulingana na mshauri wa rais Assad, Abdelkader Azouz.

"Nchi imechukua hatua tangu asubuhi ya Jumatatu. Rais Bashar al-Assad aliitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri ili kuandaa mpango wa dharura wa ngazi ya serikali, na kuwaagiza mawaziri wote na idara zinazohusika kuchukua hatua zote ili kupunguza athari mbaya za tetemeko la ardhi. Kwa sasa, serikali inahamasisha juhudi za nchi nzima kwa ajili ya uokoaji," alisema Azouz.

Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus ana wasiwasi kwamba muda unakwenda mbio na huenda hata wale wanaohofiwa kukwama kwenye vifusi wasiokolewe wakiwa hai. Mesut Hancer aliyekuwa amekaa juu ya kifusi kilichofunikwa na theluji huku akiwa ameshikilia mkono wa bintiye wa miaka 15 aliyekwama chini ya kifusi hicho katika mji wa Kahramanmaras huko Uturuki, kwa huzuni anaonekana kukata tamaa kabisa. Anasema tayari wamechelewa.

Baridi na mvua vinawatesa manusuru kuanzia watoto hadi wazee ambao sasa wanaishi kwenye majengo ya shule na hata kwenye mabasi, na ili kujitafutia joto wengi wanachoma mabaki ya mbao za nyumba zilizoanguka. Hali inazidi kuwa tete, wakati wengi wakihofu misaada inawafikia taratibu.

Mataifa mengi ikiwa ni pamoja na Marekani, China na Mataifa ya Ghuba tayari yameaanza kupeleka misaada ya kiutu na vikosi vya uokozi, wakati WHO ikikisia karibu watu milioni 23 huenda wameathiriwa na tetemeko hilo na kuyatolea wito mataifa kuharakisha zaidi ufikishwaji wa misaada.

Soma Zaidi: Idadi ya waliokufa kufuatia mitetemeko ya ardhi Uturuki na Syria imepindukia watu 5,000