Usitishwaji mapigano waanza kutekelezwa Yemen | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Usitishwaji mapigano waanza kutekelezwa Yemen

Pande zinazozozana katika mzozo wa Yemen zimeahidi kuuheshimu mpango wa kusitisha mapigano uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa ambao umeanza kutekelezwa usiku wa manane

Hatua hiyo imeongeza matumaini ya kuandaliwa duru mpya ya mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kudumu wa amani.

Mkuu wa majeshi wa vikosi vinavyomuunga mkono Rais Abedrabbo Mansour Hadi amesema “makubaliano ya kusitisha mapigano yameanza kutekelezwa” licha ya makabiliano makali katika maeneo karibu na mji mkuu Sanaa saa chache kabla ya muda wa mwisho jana usiku. Jenerali Mohamed Ali al-Makdashi amesema watauheshimu mpango huo mradi tu waasi wa Houthi wasiuvunje.

Mzozo wa Yemen umesababisha vifo vya maelfu ya watu, na kuwaacha wengine milioni 2.4 bila makaazi lakini kuna matumaini mapya kuwa mpango wa karibuni wa kuweka chini silaha unaweza kuwa jiwe la msingi la kupatikana muafaka wa amani ya kudumu ambao unaweza kufikiwa na wajumbe wa pande zote mbili katika mazungumzo yanayotarajiwa kuandaliwa prili 18 nchini Kuwait.

Shiiten Jemen Houthis

Wapiganaji wa Houthi wameyateka maeneo ya Syria

Haya hapa baadhi ya maoni ya wakaazi wa Sanaa. Abdullah Al Kowkabani anasema "inajulikana kuwa Wayemeni wa vizazi vyote wanaunga mkono amani na kumalizika vita, lakini pia sisi ni wapiganaji na tunataka huu uwe mpango sawa wa amani na sio mpango wa kujisalimisha, ili mafanikio yarejee Yemen na maadui wa Yemen watajua Yemen inaweza kuwa na amani lakini pia inaweza kupigana".

Mkaazi mwingine wa Sanaa, Marwan al Dumaini anasema "Kusitishwa mapigano kutategemea nia ya pande zote ambazo zimukabali mpango huo, ikiwa wana mapenzi kwa nchi na ikiwa nia yao ni nzuri na kwa maslahi ya watu kutokana na mateso yao katika mwaka mmoja uliopita. Tunatumai wana maazimio mazuri ya maslahi ya watu".

Majaribio matatu ya awali ya kusitisha mapigano yalivunjika baada ya jeshi la muungano linaloongozwa na Saudi Arabia kuanzisha mashambulizi mnamo Machi mwaka jana ili kuiunga mkono serikali ya Rais Hadi na kuwasogeza nyuma waasi wa Houthi wa madhehebu ya Shia ambao waliuvamia mji mkuu mwezi Septemba 2014 kabla ya kuingia katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Tangu wakati huo, vurugu na mateso vimetawala, na wapiganaji wa Jihadi likiwemo kundi la al-Qaeda katika rasi ya Uarabuni – AQAP limetumia fursa hiyo kuyakamata maeneo na kuongeza msukumo katika juhudi za amani za kimataifa.

Waasi wa houthi wanaoungwa mkono na Iran pamoja na wanajeshi walio watiifu kwa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh, wameutumia barua Umoja wa Mataifa wakiahidi kuuheshimu mpango huo kwa kusitisha operesheni za kijeshi za nchi kavu, majini na angani. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ismail Ould Cheikh Ahmed ameukaribisha mpango huo akizitaka pande zote kuuheshimu. Tofauti na majaribio ya awali ya kusitisha mapigano, baadhi ya viongozi wa Kihouthi walikutana na wanajeshi watiifu kwenye kamati ya pamoja ya kuhakikisha kuwa pande zote zinautekeleza mpango huo. Mjini Sanaa, kuna wanaoelezea mashaka kuwa Saudia itayaheshimu makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com