1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mapigano makali yaendelea kushuhudiwa Sudan

Grace Kabogo
4 Mei 2023

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku saba yaliyoanza kutekelezwa Alhamisi Sudan tayari yamevunjika baada ya mashambulizi ya anga na makombora kuripotiwa asubuhi karibu na makaazi ya rais kwenye mji mkuu, Khartoum.

https://p.dw.com/p/4QssL
Sudan Khartum | Geschlossenes Geschäft
Picha: Mohamed Khidir/Xinhua/picture alliance

Tangu mapigano yalipozuka nchini Sudan kati ya majenerali wawili wanaohasimiana takribani wiki tatu zilizopita, makubaliano ya kusitisha mapigano ya hadi saa 72 ambayo yamejadiliwa mara kwa mara, yamevunjika bila ya kutekelezwa. Usitishaji wa mapigano uliokubaliwa na pande hasimu kwa wiki nzima, ulitakiwa kuanza rasmi leo hadi Mei 11. Hata hivyo, uwezekano wa kutekelezwa kwa makubaliano hayo ni mdogo.

Mapigano yameripotiwa pia Omdurman

Mapigano hayo yameshuhudiwa wakati ambapo jeshi rasmi la Sudan limekuwa likijaribu kukisukuma nyuma kikosi maalum cha wanamgambo wa RSF, kutoka kwenye maeneo ya karibu na ikulu ya rais pamoja na makao makuu ya jeshi. Aidha, watu walioshuhudia wamesema kuwa milio ya risasi imesikika pia katika mji jirani wa Omdurman.

Kila upande unaonekana kupambana ili kuudhibiti mji mkuu wa Khartoum, kabla ya kuwepo uwezekano wowote ule wa kufanyika mazungumzo. Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Abdel Fattah al-Burhan na kamanda mkuu wa kikosi cha RSF, Mohammed Hamdan Daglo, bado hawajaonesha nia madhubuti ya kufanya mazungumzo baada ya wiki mbili za mapigano.

Somalia Mogadischu Besuch UN-Generalsekretär Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres Picha: FEISAL OMAR/REUTERS

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema jumuia ya kimataifa imeshindwa kuisaidia Sudan na ghasia nchini humo zinapaswa kumalizwa.

Akizungumza Jumatano katika ziara yake nchini Kenya, Guterres ameonya kuwa wananchi wa Sudan wanakabiliwa na janga la kibinaadamu na kwamba misaada inapaswa kuruhusiwa kuingia Sudan kwa ajili ya kuwasambazia watu wenye uhitaji zaidi.

Miundombinu ya kiraia ilindwe

''Raia na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe. Na wafanyakazi wa mashirika ya kiutu na mali zao lazima ziheshimiwe. Ninatoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuwasaidia watu wa Sudan katika harakati zao za kutafuta amani na kurejea kwa kipindi cha mpito cha kidemokrasia,'' alisisitiza Guterres.

Kwa mujibu wa Guterres bado hawajaona usitishaji wowote wa vita ukiendelea Sudan. Amesema Umoja wa Mataifa umekuwa ukishirikiana kwa karibu na Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD kushinikiza kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yatakayokuwa na ufanisi.

Sudan Konflitk l Flüchtende von Khartum auf ihrem Weg nach Ägypten
Wananchi wa Sudan wakiyakimbia mapiganoPicha: Heba Fouad/REUTERS

Hayo yanajiri wakati ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League wanakutana Jumapili ijayo kuijadili Sudan.

Mwanadiplomasia ambaye hakutaka kutajwa jina ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba mkutano huo utafanyika kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa ya Kiarabu uliopangwa kufanyika kwenye mji wa Jeddah, Saudi Arabia Mei 19.

Watu 550 wameuawa

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na wizara ya afya zinaeleza kuwa takribani watu 550 wameuawa na wengine 4,926 wamejeruhiwa tangu yalipozuka mapigano nchini Sudan.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi limesema zaidi ya watu 100,000 wameyakimbia makaazi yao na wengine 800,000 huenda wakaikimbia Sudan katika siku na wiki zinazokuja.

(DPA, AFP, Reuters)