1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usawa wa kijinsia makazini utachukua miaka 200

Yusra Buwayhid
18 Desemba 2018

Ripoti mpya iliyotolewa Jumanne na Kongamano la Uchumi la Dunia (WEF) imesema itachukua karne kadhaa hadi pale wanawake watakapoweza kupata haki sawa kama wanaume katika maeneo ya kazi kote duniani.

https://p.dw.com/p/3AHwW
Symbolbild Gehalt nach Geschlechtern
Picha: picture-alliance/dpa/A.Warnecke

Ripoti hiyo iliyotolewa leo imeonya juu ya kupungua kwa ushiriki wa wanawake katika nyanja za siasa, ukosefu wa usawa katika afya na elimu. Ujerumani imeshika nafasi ya 14 katika usawa wa mishahara kati ya wanawake na wanaume huku Marekani ikiwa imeshika nafasi ya 51.

WEF imesema kwamba itachukua karne kadhaa hadi pale wanawake watakapoweza kupata haki sawa kama wanaume katika maeneo ya kazi kote duniani. Ripoti hiyo imeeleza kwamba pengo liliopo kati ya wanawake na wanaume halitozibika kwa miaka mengine 108, na inatarajiwa kuchukua miaka 202 kuziba pengo hilo la kijinsia katika mazingira ya kazi.

"Pengo la wastani la tofauti ya mishahara kijinsia ni la asilimia 21, na kuna sababu nyingi ambazo ni za kimfumo. Ikiwa ni pamoja na kazi za vinbarua na mtazamo wa kibaguzi wa nafasi ya mwanamke katika jamii. Ukiziondoa sababu hizo na ukazitahmini kiundani zaidi unabakiwa na pengo la asilimia 2 hadi nane amabyo haiwezi kuelezwa. Na kwetu sisi ni muhimu sana kwamba tuanze kuzishughulikia hizi sababu za kimfumo," amesema mwanauchumi Henrike von Platen wakati akizungumza na DW juu ya tofauti ya mishahara kati ya wanawake na wanaume.

Infografik BTW 2017 Gender wage gap in Germany ENG
Takwimu za nchini Ujerumani za malipo kati ya wanawake na wanaumePicha: DW

Marekani ipo nyuma ya mataifa ya Ulaya

Nchi za kaskazini mwa Ulaya zinaongoza zaidi. Wanawake na wanume wana usawa zaidi nchini Iceland, ikifuata Norway, Sweden na Finland. Kwa upande mwengine, Syria, Iraq na Pakistan zinashika mkia zikiongozwa na Yemen ambayo imedhihirika kuwa kuna pengo kubwa katika usawa wa wanawake na wanaume.

Miongoni mwa mataifa 20 yanayoongoza kiuchumi, Ufaransa inaongoza, na kushika nafasi ya 12, ikifuatia Ujerumani ambayo imeshika na nafasi ya 14, Uingereza nafasi ya 15, Canada nafasi ya 16 na Afrika Kusini ya 19.

Marekani hata hivyo inaendelea kuwa nyuma katika nafasi ya 51, na ripoti inayoonyesha hivi karibuni kushuka kwa usawa wa kijinsia katika nafasi za ngazi ya waziri.

Ripoti hiyo imehitimisha kwamba hamna nchi ambayo imefanikiwa kuziba pengo la tofauti ya mishahara kati ya wanawake na wanaume na kwamba pengo hilo kimataifa ni la asilimia 51.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga