Urusi yataka mazungumzo na jeshi la Marekani kuhusu Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi yataka mazungumzo na jeshi la Marekani kuhusu Syria

Urusi inataka mazungumzo na jeshi la Marekani kuhusu mzozo wa Syria. Wakati huo huo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria anakwenda Damascus leo kujadili njia za kutafuta amani.

USA John Kerry bei einer Rede zum Nuklearabkommen mit Iran

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema Urusi inataka mazungumzo na jeshi la Marekani kuhakikisha vikosi vya nchi hizo havitumbukii katika mgogoro nchini Syria. Ikulu ya Marekani, wizara ya mambo ya nje na wizara ya ulinzi, Pentagon, zinalitathmini pendekezo hilo na Kerry amesema analiunga mkono.

Waziri Kerry amesema vita nchini Syria lazima vikome ili kulikabili wimbi la Wasyria wanaoikimbia nchi hiyo. "Kazi hiyo haiwezi kukamilika kupitia harakati ya kijeshi pekee. Ndio maana tunaendelea kufanya kazi kwa bidii kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo huu litakalosaidia kuleta utawala wa mpito kuelekea serikali itakayowajali raia, kudumisha amani na uthabiti na kuiungansha Syria kuwa taifa moja."

Marekani ilisitisha mazungumzo ya kijeshi na Urusi Machi 2014 baada ya vikosi vya Urusi kushutumiwa kwa kuingilia kati nchini Ukraine na kuwasaidia waasi katika eneo la mashariki.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameikosoa Urusi kwa kuimarisha uwepo wake Syria na kuyataka mataifa makubwa yaungane pamoja katika juhudi za amani.

Kerry atazuru barani Ulaya mwishoni mwa juma kukutana na washirika muhimu kuujadili mzozo wa Syria pamoja na masuala mengine nyeti huku Urusi ikiendelea kuimarisha uwepo wake kijeshi nchini humo.

Russland Sergej Lawrow

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov

Jana alizungumza na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov kwa mara ya tatu kwa njia ya simu. "Niliweka wazi kuwa hatua ya Urusi kuendelea kumsaidia Assad kunahatarisha kuuchochea mzozo na kuhujumu lengo letu la pamoja la kupambana na itikadi kali kama hatutaelekeza nguvu katika kutafuta suluhisho la amani."

Baraza la usalama liwasaidie Wasyria

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinaadamu na mratibu wa misaada ya dharura, Stephen O'Brian, amelitaka baraza la usalama kuwasaida Wasyria.

"Baraza hili linalazimika kuelekeza juhudi zake katika kutafuta suluhisho la kisiasa. Nalitaka tena baraza hili limalize tofauti zake na lishirikiane pamoja kumaliza jinamizi linalowakabili raia wa Syria. Natumai kwa masilahi ya Wasyria suluhisho la kisasa litapatikana haraka iwezekanavyo."

Wakati haya yakiarifiwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Syria Stafffan de Mistura anakwenda Damascus leo kukutana na waziri wa kigeni Walid Muallem kwa sababu Syria inatajia majibu ya maswali kuhusu mpango wake kuelekea amani. Hii itakuwa ziara ya sita ya de Mistura Damascus, lakini ya kwanza tangu alipoikosoa Syria kuhusiana na mashambulizi 16 ya kutokea angani yaliyowaua watu karibu 100 katika mji wa Douma, karibu na mji mkuu Damascus.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/ape

Mhariri:Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com