Urusi yataka dunia iungane dhidi ya IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi yataka dunia iungane dhidi ya IS

Baada ya kuanzisha mashambulizi ya angani nchini Syria, Urusi imetoa wito kwa dunia kuungana katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, na imesambaza andiko la muswada wa azimio la UN kusaidia kufanikisha azma hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alijibu wito huo uliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov kwa kutangaza kuwa Marekani iko tayari kukaribisha hatua za Urusi nchini Syria iwapo hatua hizo zitaelekezwa kwa makundi ya Dola la Kiislamu IS na Al-Qaeda, na kuahidi kuwa muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya IS nchini Syria utaongeza pakubwa juhudi zake.

Waziri Lavrov alisema yeye na waziri Kerry bado wanatofautiana kimtazamo kuhusu suluhu ya mgogoro wa Syria lakini wamekubaliana kutafuta njia za kuanza mchakato wa kisiasa. "Sote tunataka Syria inayofuata demokrasia, iliyoungana, isiyoegemea dini na ambayo ni nyumbani kwa makundi yote ya kikabila na kiimani ambayo haki zake zinalindwa, lakini tunatofautiana juu ya namna ya kufika huko. Lakini tumekubliana juu ya baadhi ya hatua za kuweka mazingira ya kuwezesha mchakato wa kisisasa," alisema Lavrov.

Moja ya shambulizi lililofanywa na ndege za Urusi nchini Syria.

Moja ya shambulizi lililofanywa na ndege za Urusi nchini Syria.

Syria yaiunga mkono Urusi

Muswada wa Urusi unayatolewa mwito mataifa kuratibu shughuli zao kwa ridhaa ya serikali za mataifa katika eneo zinakofanyika shughuli hizo. Lugha ya muswada huo, ambayo inamaanisha serikali ya Syria, inafanana na ile iliyotumika katika muswada wa awali wa taarifa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa na Urusi lakini Marekani ikakataa kuujadili.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Wallid al Muallem aliliambia baraza la usalama kuwa nchi yake inaridhia kwa dhati hatua za Urusi na kuyaita mashambulizi ya Ufaransa na mengine nchini Syria yasiyoihusisha serikali yake kuwa ukiukaji wa dhahiri wa sheria za kimataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif , mshirika wa karibu zaidi wa utawala mjini Damascus, alibainisha kuwa muungano unaoongozwa na Marekani ulikuwa unashindwa kufikia malengo yake.

Marekani kuzungumza na Urusi

Waziri Lavrov alisema Urusi iko tayari kuweka njia za kudumu za mawasiliano kuhakikisha mapambano hayo yanafanikiwa. Alizitaja nchi zenye dhima kubwa katika kutatua mgogoro wa Syria zikiwemo Iran, Urusi, Saudi Arabia, Uturuki, Misri, Jordan, Qatar, Marekani na hata China. Alisema wanachokihitaji ni mikakati ya pamoja inayoungwa mkono na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais wa Syria Bashar al-Assad akizungumza na wanajeshi wake walioko kwenye uwanja wa mapambano.

Rais wa Syria Bashar al-Assad akizungumza na wanajeshi wake walioko kwenye uwanja wa mapambano.

Waziri John Kerry alisema Marekani iko tayari kufanya kile alichokiita mazungumzo ya kuondoa mgogoro na Urusi kuhusiana na kampeni mbili za mashambulizi haraka iwezekanavyo. "Tumekubaliana hata kama bado hatujapata azimio kuhusiana na chaguo muhimu katika suluhu ya kisiasa, kwamba kuna hatua makhsusi zinazoweza kusaidia kutuongoza katika mwelekeo sahihi."

Balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa Abdallah Al-Mouallimi, aliyatuhumu mashambulizi ya Urusi kwa kulenga maeneo ambako hakuna wapiganaji wa Daesh au Dola la Kiislamu, na kusababisha vifo vya raia wasiyo na hatia -- tuhuma ambazo hata hivyo zimekanushwa na waziri Sergei Lavrov.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius, ambaye nchi yake ilianzisha mashambulizi ndani ya Syria siku chache zilizopita, aliliambia baraza kuwa Ufaransa iko tayari kushirkiana na Urusi kwa masharti ya kukomesha vurugu dhidi ya raia wa Syria, waweke bayana kabisaa nani mataifa yanapambana naye na kuondoka kwa rais Bashar al Assad-

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape, afpe,

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com