1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasita kushambulia viwanda, Ukraine

Lilian Mtono
21 Aprili 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameviagiza vikosi vyake kusitisha mipango ya kushambulia kiwanda cha Azovstal kilichopo katika mji wa Mariupol nchini Ukraine, na badala yake walilinde eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4ACor
Präsident Putin am 5. April 2022
Picha: Mikhail Klimentyev/Kremlin/SputnikREUTERS

Kiongozi huyo wa Urusi Vladimir Putin amesema anataka kiwanda hicho cha Azovstal kiendelee kulindwa na kuwa salama. Anatoa maagizo hayo wakati polisi nchini Ukraine wakiarifu kupata miili tisa ya raia, katika mji wa Borodyanka karibu na Kyiv, iliyokuwa na alama za kuteswa. 

Rais Vladimir Putin ametoa maagizo hayo kwa waziri wake wa ulinzi Sergei Shoigu kwenye mkutano uliorushwa kupitia televisheni akisema haoni umuhimu wa kulishambulia eneo hilo la viwanda na badala yake lifungwe kiasi cha hata nzi kushindwa kutoka,.

Putin aidha ameikaribisha taarifa ya Shoigu kwamba majeshi ya Moscow yamedhibiti kikamilifu eneo lililobakia kwenye jiji la Mariupol ingawa Ukraine yenyewe haijasema chochote kuhusiana na madai haya ya karibuni. Waziri huyo hapo kabla alimwambia Putin kwamba wanajeshi zaidi ya 2,000 wa Ukraine bado walikuwa wamejificha kwenye eneo hilo la viwanda.

Ukraine Krieg | Mariupol
Uharibifu unaoonekana katika mji wa Mariupol nchini UkrainePicha: Maximilian Clarke/ZUMA Wire/IMAGO

Rais Putin amesifu ushindi huo aliouita mkubwa na wa kimkakati, utakaowasaidia kujiunganisha na eneo ililolinyakua la Crimea hadi maeneo ya waasi wanaopigania kujitenga na Ukraine na wanaoungwa mkono na Urusi.

Hatua ya kutolishambulia eneo hilo, inaifanya Urusi kushindwa kutangaza ushindi kamili kwenye mji huo wa Mariupol na kulingana na Shoigu, eneo hilo sasa lina ulinzi na ni salama.

Miili mingine yapatikana katika kaburi la pamoja, Ukraine.

Jijini Kyiv, waziri mkuu wa Uhispania Pero Sanchez na Mette Frederiksen wa Denmark wanakuwa viongozi wa hivi karibuni kutoka Ulaya kuonyesha kuiunga mkono Ukraine wakati wanapozuru nchi hiyo. Viongozi hao watakutana na rais Volodymir Zelenskyy aliyeonya kwenye hotuba yake ya video usiku wa jana kwamba Urusi haijaachana na majaribio yake ya kuanzisha mashambulizi mapya na makubwa zaidi.

Dänemark | Mette Frederiksen
Waziri mkuu wa denmar Mette Frederiksen, anazuru Ukraine akiwa mmoja wa viongozi wa karibuni wa Ulaya kuzuru Ukraine hivi karibuni.Picha: Ólafur Steinar Rye Gestsso/Ritzau Scanpix/AP/dpa/picture alliance

Frederiksen alinukuliwa kwenye taarifa yake akisema Magharibi inawaunga mkono watu wa Ukraine. Kulingana na shirika la habari la Europa, waziri mkuu Sanchez kwa upande wake alisema anataka kutumia ziara hiyo kuelezea uungwaji mkono wa Uhispania kwa watu wa Ukraine, pamoja na matamanio yake ya amani. Anatarajiwa pia kuufungua tena ubalozi wao nchini Ukraine.

Wakati wasiwasi ukizidi kuongezeka kwa watu wa Mariupol, mkuu wa polisi katika eneo la Kyiv amesema leo kwamba wamegundua makaburi mawili ya pamoja katika mji wa Borodyanka karibu na Kyiv ambamo walikuta miili tisa.

Soma Zaidi:Biden amtuhumu Putin kwa mauaji ya halaiki nchini Ukraine 

Mkuu huyo wa polisi Andriy Nebytov amesema kupitia ukurasa wa Facebook kwamba miongoni mwa miili hiyo ni wanawake wawili na kijana wanaodhaniwa kuuawa na wavamizi wa Urusi. Amesema baadhi ya miili ilikuwa na alama za kuteswa.

Mashirika: APE/AFPE/DPAE