1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yawataka tena wanajeshi wa Ukraine kujisalimisha

Mohammed Khelef
19 Aprili 2022

Kwa mara nyengine tena, jeshi la Urusi limewataka wanajeshi wa Ukraine katika mji uliozingirwa wa Mariupol kujisalimisha kabla ya eneo walilojificha kushambuliwa, huku ikizidisha mashambulizi yake kwenye miji mingine.

https://p.dw.com/p/4A5nl
Ukraine | Evakuierung eines Hospitz in Chasiv Yar
Picha: Petros Giannakouris/AP/picture alliance

Asubuhi ya Jumanne (Aprili 19), Kanali Jenerali Mikhail Mizintsev wa Urusi aliwapa wanajeshi wa Ukraine waliojificha kwenye kiwanda kikubwa kabisa cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol hadi mchana wawe wameshajisalimisha, akisema wale ambao wangelifanya hivyo wangeliepuka kushambuliwa.

Wito wa mkuu huyo wa operesheni ya kijeshi ya Urusi ulikuja ikiwa ni zaidi ya masaa 24 tangu muda wa mwisho uliokuwa umewekwa na Urusi kupita bila wanajeshi hao wa Ukraine, ambao wamekuwa wakijaribu kwa wiki saba mfululizo kuulinda mji wao usitekwe, kutii amri hiyo. 

Kiwanda cha chuma cha Azovstal, ambacho kina kilomita 11 za mraba, ni ngome ya mwisho ya wanajeshi wa Ukraine waliosalia katika mji wa Mariupol ambao una bandari ya kimkakati ya Bahari ya Azov.

Urusi yataka kuchukuwa Donbas yote

Ukraine, Hostomel | Ein Soldat sammelt nicht explodierte Granaten
Mabomu yaliyokuwa hayajaripuka karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Awali, mkuu wa majeshi wa Ukraine alisema vikosi vya Urusi sasa vilikuwa vinaelekeza juhudi zao kwenye kuchukuwa udhibiti kamili wa mikoa ya Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine. 

"Awamu mpya ya vita ilianza jana Jumatatu, ambapo wavamizi walijaribu kuvunja ngome yetu kwenye takribani eneo zima la mstari wa mbele katika mikoa ya Donetsk, Luhansk na Kharkiv." Ilisema taarifa ya mkuu huyo wa majeshi.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa jeshi la Urusi limeendelea na kuuzingira na kuushambulia mji wa Mariupol na kuangusha makombora kutoka angani katika miji mingine.

Katika mji wa Kreminna ulio mashariki mwa Ukraine, mapigano yalianza mapema asubuhi ya Jumanne na kukwamisha juhudi za kuwaokowa raia waliokwama.

Kwa mujibu wa jeshi la Ukraine, hiyo ni sehemu moja ya kati ya mbili, ambazo ndizo pekee Warusi walizojaribu kuzivamia tangu jana.

Mji wa Luhansk wachukuliwa na Urusi

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine | Zerstörung in der Region Mykolajiw
Kituo cha michezo katika kijiji cha Luch baada ya mashambulizi ya Urusi mkoani Mykolaiv, Ukraine.Picha: Celestino Arce Lavin/ZUMA Press/picture alliance

Mtawala wa kijeshi wa Luhansk, Serhiy Haidai, alisema kuwa mji huo ulishambuliwa kwa makombora usiku mzima, ambapo majengo saba yanayokaliwa na raia yameunguwa moto, na kwamba uwanja wa Olimpiki ulishambuliwa.

Haidai alisema baadaye kwenye kituo cha televisheni cha Ukraine kwamba wanajeshi wa Urusi walitwaa udhibiti wa mji huo baada ya kuangamiza kila kitu, na hivyo wanajeshi wake wakalazimika kurudi nyuma, kujipanga upya na mapambano.

Makombora ya Urusi yaliangukia pia katika mji wa Lviv, mbali ya miji mingine mingi ya Ukraine usiku kuamkia Jumanne.

Yenyewe Urusi ilisema makombora yake yalipiga zaidi ya maeneo 20 ya kijeshi, yakiwemo maghala ya silaha, magari na makao makuu ya kamandi za kijeshi, huku ndege zake zikishambulia maeneo 108.