1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yapongeza mkutano wa Biden na Putin

Josephat Charo
17 Juni 2021

Utawala wa Kremlin umeipongeza na kuikaribisha hatua ya rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kufanya mdahalo juu ya uthabiti wa kimkakati na udhibiti wa silaha.

https://p.dw.com/p/3v72z
Schweiz l Biden und Putin treffen sich in Genf l Verabschiedung Putin
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Denis Balibouse/REUTERS/AP/picture alliance

Utawala wa Kremlin uliupongeza mkutano kati ya Putin na Biden ukisema umeleta tija kubwa. Marais hao walitoa taarifa fupi kufuatia mkutano wao wa ana kwa ana jana mjini Geneva, wakisema wamekubaliana kuanza mdahalo kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia.

Msemaji wa rais Putin, Dmitry Peskov alilipongeza tamko la pamoja la viongozi hao kuhusu mazungumzo ya kimkakati ya udhibiti wa silaha. Akizungumza kwenye mahojiano na redio Ekho Moskvy hivi leo Peskov, alisema japo taarifa hiyo ilikuwa fupi sana, tamka lao la pamoja linatambua majukumu muhimu ya mataifa yao mawili, sio tu kwa wananchi wao, bali pia kwa ulimwengu wote kwa ujumla.

Peskov alisema tangia mwanzo walitahadharisha juu ya kuwa na matarajio makubwa kuhusu mkutano wa kilele kati ya Biden na Putin, lakini sasa kwa tathmini ya rais Putin mwenyewe, ulikuwa mkutano wenye mafanikio makubwa.

Hata hivyo Peskov alisema bado kuna tofauti kati ya mataifa hayo, kwa mfano kuhusu suala la Belarus au jukumu la jumuiya ya kujihami ya NATO.

"Tulisikia wakati wa ziara ya Ulaya ya rais Biden akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu uwezekano wa kuipa Ukraine uanachama wa NATO. Hili lilisemwa kwa mara ya kwanza katika ngazi ya juu kabisa na bila shaka, linatutia wasiwasi," akaongeza Peskov.

Balozi kufunguliwa tena

Msemaji huyo wa Kremlin pia alitangaza kurejea kwa balozi wa Urusi mjini Washington katika siku zijazo. Putin na Biden waliafikiana kuhusu suala hili katika mkutano wao wa Geneva. Mabalozi wa nchi hizo mbili walirejeshwa nyumbani wakati wa msimu wa machipuko mwaka uliopita wakati msuguano ulipozidi baina ya Urusi na Marekani.

USA-Russland-Gipfel in Genf | Joe Biden
Rais Joe Biden wa MarekaniPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Mapema leo naibu waziri wa nchi za nje wa Urusi, Sergei Ryabkov alisema hatua ya pande hizo mbili kukataa vita vya nyuklia ndiyo ufanisi halisi. Utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ulijitoa kwenye mikataba kadhaa ya kimataifa, ukiwemo mkataba wa kudhibiti silaha za nyuklia za masafa ya kati na urusi, INF.

Ryabkov alisema tangu kurefushwa kwa mkataba mpya wa kudhibiti silaha za nyuklia wa START chini ya utawala wa Biden, hii ni hatua ya pili ya serikali ya mjini Washington kurejesha utumiaji wa akili na busara na mtazamo wa uwajibikaji na kubeba dhamana kuhusiana na masuala muhimu ya usalama wa kimataifa.

Mkataba mpya wa START ndio wa mwisho uliosalia kati ya mataifa hayo mawili yenye silaha za nyuklia yanayohodhi zaidi ya asilimia 90 ya silaha zote za nyuklia duniani.

Kwa mujibu wa Ryabkov, mdahalo kuhusu uthabiti wa kimkakati kati ya Urusi na Marekani unatakiwa kuanza katika wiki chache zijazo na sio miezi.

(afp, reuters)