1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

​​​​​​​Urusi tayari kuandaa Kombe la Dunia

3 Julai 2017

Dimba la Kombe la Mabara limekuwa ni majaribio ya kufana yanayoonyesha uwezo wa Urusi kuandaa tamasha kubwa kabisa la Kombe la Dunia mwaka ujao. Urusi na FIFA zimeridhika na namna mambo yanavyokwenda

https://p.dw.com/p/2fqtr
Russland FIFA Maskottchen 2018
Picha: picture alliance/dpa/M. Pochuyev

Wakati Kombe la Mabara lilizishirikisha timu nane katika miji minne ya Urusi, Kombe la Dunia lenye timu 32 katika miji 11 linaweka changamoto kubwa ya usafiri. Rais wa FIFA Gianni Infantino ameipongeza Urusi kwa mikakati iliyoweka. "tuliskia kuhusu vurugu kabla ya dimba, kuhusu matukio ya uhuni, ubaguzi, lakini hatujaona chochote. Kila kitu kilikwenda sawa. Tuliskia kuhusu miundo mbinu, kwamba haiku tayari, lakini mambo yamekuwa murwa kabisa, viwanja safi kabisa vya michezo".

Lilikuwa ni dimba ambalo FIFA ililitumia kuujaribisha mfumo wa video na kama ilivyodhihirika katika baadhi ya matukio, ipo kazi ya kufanywa maana kuna maamuzi yaliyochukuliwa na marefarii ambayo yalizusha gumzo. Licha ya hayo, Infantino ameusifu mfumo wa video akisema ulikuwa wenye mafanikio makubwa katika dimba hilo lakini akakiri kuwa unahitaji kuboreshwa. "Umekuwa na mafanikio makubwa kwa sabbau katika matukio mengi marefa wa kutumia video walikuwa na nafasi ya kuingilia kati, na kumsaidia mwamuzi mkuu. Na katika maamuzi sita yaliyoubadilisha mchezo mpaka sasa, mfumo wa video wa kuwasidia waamuzi ulirekebisha uamuzi au kosa lililofanywa na refarii. Hivyo bila mfumo wa video tungekuwa na dimba tofauti.

FIFA inapanga kuujaribisha zaidi na kuuimarisha mfumo huo katika ligi za Ujeruani na Ureno msimu ujao, wakati Infantino akitumai kuwa utakuwa tayari kwa ajili ya kutumiwa rasmi katika Kombe la Dunia 2018.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo