Upinzani Syria wasema lazima waungane dhidi ya vikosi vya serikali | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Upinzani Syria wasema lazima waungane dhidi ya vikosi vya serikali

Kiongozi wa kundi la upinzani Syria Abdulbaset Sieda amesema wanapaswa kuchukua jukumu muhimu katika hatua yoyote ya kuungana dhidi ya utawala wa Rais Bashar Al Assad.

Upinzani nchini Syria

Upinzani nchini Syria

Makundi kadhaa ya upinzani yanayoishi nje ya Syria yanajitayarisha kufanya mkutano wao siku ya Alhamisi wiki hii. Mkutano ambao ni wa kuonesha umoja wao na waasi wanaopigana nchini Syria. Upinzani unanuia kuungwa mkono na jamii ya kimataifa na pia kutarajia kupewa silaha za kupambana na vikosi vya serikali ya Bashar Al Assad.

Lakini dalili za mapema za mvutano katika mkutano huo wa Alhamisi utakaofanyika Doha, nchini Qatar, zimeanza kujitokeza huku kukiwepo atiati juu ya iwapo makundi hayo ya upinzani yataungana. "Tutakwenda katika mkutano huu kwa moyo mkunjufu lakini tunasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa umoja kama upinzani" Alisema kiongozi wa baraza la kitaifa la Syria SNC Abdulbaset Sieda.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov

Mkutano huo wa Alhamisi utazungumzia pia pendekezo la mwanachama wa SNC Riad Seif kuunda kundi la raia 50 ambao baadaye wataunda serikali ya muda na kushirikiana na jeshi la waasi jambo ambalo ni muhimu katika kupata uungaji mkono wa jamii ya Kimataifa.

Huku hayo yakijiri waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amewahimiza wapinzani nchini Syria kuachana kabisa na madai yao ya kutaka lazima Rais Assad aondoke madarakani kabla ya kufanyika mazungumzo yoyote ya kumaliza mgogoro wa Syria.

Akizungumza baada ya mkutano kati yake na aliyekuwa waziri mkuu wa Syria Riad Hijab aliyekimbilia Jordan mwezi wa Agosti mwaka huu, Lavrov aliushutumu upinzani kutojali maisha ya watu wa syria kwa kutaka rais Assad aondoke kwanza kabla ya juhudi za kusitisha mapigano.

Lavrov ambaye nchi yake ni mshirika mkubwa wa Syria, amesema upinzani pamoja na serikali wanapaswa kuzingatia pendekezo lililopitishwa mwezi Juni na mataifa yalio na nguvu duniani mjini Geneva. Pendekezo hilo ni la kutaka serikali ya mpito nchini Syria, japo pendekezo hilo halikuweka wazi iwapo Rais Assad angatuke madarakani.

Tangu kuanza kwa mapigano hayo takriban watu 36,000 wameuwawa nchini Syria huku wengine wengi wakipoteza makaazi yao.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron

Kwengineko waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema Rais Assad anaweza kupewa njia salama ya kuondoka Syria ikiwa atakubali kuachia madaraka. Cameron akizungumza na televisheni ya Al Arabiya amesema hatoi nafasi ya Assad kutorokea nchini Uingereza lakini akitaka kuondoka ataondoka na mipango yake ya kuondoka itapangwa. Waziri mkuu huyo wa Uingereza ambaye yuko ziarani Saudi Arabia baada ya kuwa Umoja wa Falme za kiarabu kwa ziara ya siku mbili amesema anasikitishwa kuwa hakuna zaidi kinachoweza kufanyika na kwamba utawala wa Assad Unazidi kumaliza watu wake na kukandamiza upinzani.

Mapigano zaidi Syria

Moshi uliotokana na kombora kurushwa ndani ya Syria

Moshi uliotokana na kombora kurushwa ndani ya Syria

Huku hayo yakiarifiwa nchini Syria bomu moja lililoegeshwa ndani ya gari liliripuka na kuutikisa mji wa Damascus mapema leo asubuhi. Kulingana na shirika hilo la kutetea haki za binaadamu, bomu hilo lililoripuka katika mji ulio karibu sana na mji mkuu Damascus, lilisababisha majeruhi kadhaa pamoja na uharibifu mkubwa.

Mashambulizi ya angani yalilenga pia mji wa Douma ulioko kilomita 13 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Damascus ambapo mabomu mawili yalirushwa katika jengo moja huku makombora yakiangushwa katika eneo la Al Bab katikati mwa mji wa Homs.

Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu lenye makao yake makuu mjini London limesema vikosi vya serikali vimeendelea kushambulia maneo mengine ya magharibi mwa eneo la Takia mjini Homs na Quneitra mahali ambapo jeshi la Israel lilisema siku ya Jumatatu kuwa jeshi la Syria lilishambulia gari lake la kijeshi.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa/AFP/

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com